BILIONI 568 KUNUFAISHA WABUNIFU SEKTA YA AFYA
Kutoka kulia ni Mtendaji Mkuu wa
Atamizi ya DTBi yenye lengo la kuleta mapinduzi katika Sekta ya Afya,
Mhandisi George Mulamula, Mkurugenzi wa Tume ya Sayansi na Teknolojia,
Dkt. Hassan Mshinda, Mratibu wa Kikanda wa MCC/PEPFAR Bwana Mitch
Blasser pamoja na Meneja Mkuu wa Mradi wa Data for Local Impact Innovation Challenge (DLI), Agapiti Manday wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa uzinduzi wa mradi huo.
Mkurugenzi wa Tume ya Sayansi na
Teknolojia, Dkt. Hassan Mshinda, akikabidhi Hundi ya millioni 568 kwa
wajasiriamali wavumbuzi 12 waliovumbua miradi mbalimbali ya kuiendeleza
Sekta ya Afya chini ya mradi wa Data for Local Impact Innovation Challenge
(DLI) unaofadhiliwa na Mfuko wa Rais wa Marekani katika Vita dhidi ya
Makali ya UKIMWI (PEPFAR) na kusimamiwa na taasisi ya serikali ya
marekani ya Changamoto za Millenia (MCC),
Wajasiriamali vijana 12 waliovumbua miradi mbalimbali ya kuiendeleza Sekta ya Afya chini ya mradi wa Data for Local Impact Innovation Challenge
(DLI) unaofadhiliwa na Mfuko wa Rais wa Marekani katika Vita dhidi ya
Makali ya UKIMWI (PEPFAR) na kusimamiwa na taasisi ya serikali ya
marekani ya Changamoto za Millenia (MCC) wakiwa katika picha ya pamoja
na hundi ya mfano ya millioni 568 walizokabidhiwa.
…………………………………………………………………………………..
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Tume ya Sayansi na Teknolojia
(COSTECH) inategemea kukabidhi jumla ya shilingi bilioni 568.575, 000/=
kwa vijana 12 waliobuni mawazo bora yatakayosaidia kuondoa changamoto
zinazoikabili sekta ya Afya hapa nchini.
Mkurugenzi wa Tume ya Sayansi na
Teknolojia, Dkt. Hassan Mshinda aliyasema hayo hivi karibuni Jijini Dar
es Salaam alipokuwa akizindua mradi wa Data for Local Impact Innovation Challenge
(DLI) uliopo chini ya Atamizi ya DTBi yenye lengo la kuleta mapinduzi
katika matumizi ya taarifa na takwimu mbalimbali katika sekta ya Afya.
Dkt. Mshinda alisema shughuli za
ujasiriamali na ubunifu ni muhimu na chachu ya maendeleo ya nchi yoyote
kwa kuwa zinasaidia kutengeneza ajira, kuongeza wigo wa shughuli za
uzalishaji mali pamoja na kuchangia katika pato la taifa.
Alisema Serikali kupitia COSTECH
iliamua kuanzisha Atamizi ya DTBi mwaka 2011 ili kuwasaidia
wajasiriamali wanaoshughulika na suala la TEHAMA.
“Nafahamu mradi huu umejikita
katika changamoto za matumizi ya taarifa katika sekta ya afya, maendeleo
ya kiuchumi na usawa wa kijinsia kama yalivyotanabaishwa katika malengo
ya maendeleo endelevu, ubunifu hasa katika eneo la TEHAMA ni muhimu
sana kwa sababu unasaidia kuongeza tija na ufanisi wa utoaji huduma
katika sekta mbalimbali nchini”,Alisema.
Aidha Dkt. Mshinda alisema nia ya
DTBi ni kuwawezesha Vijana, kuwajengea uwezo na kuwapa misaada ya
msingi wataalam na wabunifu wa kitanzania waliopo katika eneo la TEHAMA
ili kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ya kitanzania kwa
kutumia teknolojia.
Dkt. Mshinda aliwahakikishia
wajasiriamali hao kuwa COSTECH itaendelea na juhudi zake za
kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Serikali na taasisi za fedha
kukabiliana na changamoto ya masharti ya mikopo kwa wajasiriamali.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa
DTBi, Agapiti Manday alisema wanapokea mawazo mbalimbali ya vijana na
kuyachuja na baadae wanachukua vijana wachache walio na mawazo bora
zaidi na kuwawezesha ili waweze kuweka mawazo yao katika vitendo.
“Tunafahamu kuwa wapo vijana
wengi mtaani wanaomaliza elimu katika ngazi mbalimbali ikiwemo vyuo
vikuu ambao wana mawazo bora ya kuipeleka Tanzania mbele kimaendeleo
lakini fursa hiyo wanaikosa kutokana na kukosekana kwa fedha na miongozo
ya kuyafanya mawazo yao kuwa katika vitendo hivyo mradi huu unawasaidia
vijana kuweka mawazo kuwa vitendo,”alisema Manday.
Bw. Manday Amefafanua kuwa
changamoto kubwa ya wajasiriamali wa kitanzania ni ukosefu wa mitaji ya
kufanikishia au kuendeleza shughuli zao za kiujasiriamali hivyo kwa
kupitia mradi huo wataendelea kusaidiwa hadi pale watakapoweza kusimama
kwa nguvu zao wenyewe.
Mradi huo mpya kwa Tanzania,
umefadhiliwa na Mfuko wa Rais wa Marekani katika Vita dhidi ya Makali ya
UKIMWI (PEPFAR) na kusimamiwa na taasisi ya serikali ya marekani ya
Changamoto za Millenia (MCC), Mradi huu umeanza utekelezaji mnamo mwezi
Aprili mwaka 2016.
No comments