WAZIRI MKUU: HOSPITALI YA HAYDOM KUPANDISHWA HADHI
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mtafiti katika
hospitali ya Haydom wilayani Mbulu, Rosemary Mshama (kulia) wakati
alipotembelea Kituo cha Utafiti cha hospitali hiyo Februari 20, 2017.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama sanamu ya binadamu wakati alipotembelea
moja ya darasa la Chuo cha Uuguzi katika hospitali ya Haydom wilayani
Mbulu, Februari 20, 2017.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama sukari na nishati ya kuni
inayotengenezwa kwa kutumia makapi ya miwa inayokamuliwa katika kiwanda
cha sukari cha Manyara wakati alipotembelea kiwanda hicho Februari 19,
2017. Kuni hizo zina ubora unaofanana na ule wa makaa ya mawe na
hutumika zaidi katika mitambo inayotumia nishati ya kuni. Kulia ni
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba na kulia kwa
Waziri Mkuu, ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dkt. Joel Bendera. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akifurahia ngoma ya asili ya kabila la Wahatzabe
wakati alipowasili kwenye hospitali ya Haydom kuanza ziara ya wilaya ya
Mbulu, Februari 20, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa wilaya mstaafa, Mama
Sanka baada ya kuwasili kwenye makazi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara mjini
Babati akiwa katika ziara ya mkoa huo, Februari 19, 2017. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haina kipingamizi na wazo la
kuifanya hospitali ya rufaa ya Haydom kuwa ya kanda kwani hatua hiyo
itaupunguzia mzigo Serikali.
“Serikali
hii ni sikivu, na kuifanya hospitali hii kuwa ya kanda ni kazi ndogo.
Kwa hiyo nitamleta Waziri wa Afya aje awaongoze kusimamia vigezo vya
kuifanya hospitali hii iwe ya kanda,” amesema.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumatatu, Februari 20, 2017) wakati akizungumza
na mamia ya wakazi wa kata ya Haydom kwenye mkutano wa hadhara
uliofanyika kwenye uwanja wa kata.
"Serikali
haina kipingamizi na wazo lenu, cha msingi ni vigezo muhimu vifuatwe.
Kwa hiyo, nitamleta Waziri wa Afya awasaidie kuangalia vigezo,"
amesisitiza.
“Kama
vigezo havipo, tushirikiane kuvikamilisha kwa sababu uwepo wa hospitali
hii kwa hadhi ya kanda kunaisadia Serikali kutokana na nafasi yake
kijiografia,” amesema Waziri Mkuu
“Nia
yetu ni kupunguza gharama kwa mgonjwa anayelazimika kutoka Simiyu hadi
Bugando (Mwanza) au kutoka Arusha hadi Muhimbili (Dar es Salaam). Hapa
ni katikati na nimearifiwa kuwa wagonjwa kutoka mikoa mitano ya Tabora,
Simiyu, Arusha, Singida na Manyara wanafika hapa kupatiwa matibabu,”
amesema.
Amesema
Serikali imepokea maombi kwa ajili ya watumishi wanaotakiwa kwenye
hospitali hiyo na kwamba hivi karibuni itaajiri watumishi kati ya 5,000
hadi 6,000 wa sekta ya afya peke yake. “Tumekwishaanza kuajiri, tumeanza
na sekta ya elimu kwa kuajiri walimu 4,693 ambao wote ni wa fani ya
sayansi. Na sekta inayofuata ni ya afya, kwa hiyo hao watumishi 90
wanaohitajika watapatikana kwenye kundi hilo hilo,” amesema.
Hospitali hiyo inahudumia wananchi kutoka wilaya nane za Mbulu, Hanang, Babati, Karatu, Mkalama, Iramba, Kondoa na Meatu.
Wakati huohuo, Balozi
wa Norway nchini Tanzania, Bibi Hannamarie Kaarstad ambaye alikuwepo
kwenye mkutano huo, alisema amefarijika na mchango unaotolewa na
Serikali ya Tanzania kusaidia juhudi zinazofanywa na marafiki wa
hospitali walioko Norway.
“Hospitali
ya Haydom ni mahali thabiti ambapo mshikamano baina ya Tanzania na
Norway unaweza kuonekana kwa dhahiri. Nawashukuru watumishi wa hospitali
kwa moyo wao wa kujitoa kuwahudumia wananchi wa wilaya ya Mbulu na
maeneo ya jirani,” amesema.
Hospitali
hiyo ambayo inaendeshwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT) Dayosisi ya Mbulu kwa ufadhili kutoka Serikali za Tanzania na
Norway, ilianzishwa mwaka 1955 ikiwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 50.
Hivi sasa ina uwezo wa kulaza wagonjwa 420 kwa wakati mmoja.
Pia
inatoa huduma za upasuaji, magonjwa ya macho, tiba ya mifupa na mazoezi
ya viungo. Ilipandishwa hadhi kuwa ya rufaa baada ya mkoa wa Manyara
kuanzishwa.
Mapema, akisoma
taarifa kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa Tiba wa hospitali hiyo,
Dk. Emanuel Q. Nuwass alisema wameomba kibali cha ajira kwa watumishi
90 kupitia bajeti ya mwaka 2016/2017.
“Tumeomba
pia hospitali ipandishwe hadhi na kuwa ya rufaa ya kanda (Kaskazini
kati au Kanda maalum) ili iweze kutoa huduma bora kwa mkoa wa Manyara na
mikoa jirani kwani wahisani wa maendeleo wako tayari kuchangia ujenzi
wa miundombinu,” alisema.
Pia aliomba waongezewe ruzuku ya dawa ikilinganishwa na ya sasa hivi ambayo ni asilimia 15 na pia waongezwe malipo ya on call allowancekwa ajili ya madaktari na watumishi wengine wa hospitali hiyo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, FEBRUARI 20, 2017.
No comments