WAZIRI MKUU AKABIDHIWA KAZI YA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na
Mawaziri na Makatibu Wakuu baada ya kuwaapisha Mabalozi na Kamishna Mkuu
wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Ikulu Jijini Dar
es Salaam.
PICHA NA HASSAN SILAYO-MAELEZO
……………………………………………………………………
Jacquiline Mrisho na Eliphace Marwa – MAELEZO.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amemkabidhi Waziri Mkuu, Mhe. Kassim
Majaliwa kazi ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya akiwa kama
Mwenyekiti wa Tume ya Kudhibiti Dawa hizo nchini.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo
Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati akiwaapisha Kamishna Jenerali wa Jeshi
la Uhamiaji, Anna Peter Makakala, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na
Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers William Sianga pamoja na mabalozi
watatu Mhe. Omary Yusuph Mzee, Mhe.Joseph Edward Sokoine pamoja na Mhe.
Grace Aron Mgovano aliowateua hivi karibuni.
Dkt. Magufuli amesema kuwa Waziri
Mkuu anatajwa kwenye Sheria Na.5 ya mwaka 2015 kuwa ni Mwenyekiti wa
Tume hiyo ambapo Wajumbe wake ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa Elimu ana Mafunzo ya
Ufundi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Waziri wa Fedha na Mipango, Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Waziri wa
Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
“Nalipongeza sana Bunge la
kipindi cha mwaka 2010 – 2015 chini ya Spika mstaafu, Mhe. Anne Makinda
lililopitisha Sheria hii baada ya kuona sheria za mwanzo za kupambana na
dawa za kulevya hazina nguvu hivyo Wabunge wa wakati ule walisimama kwa
pamoja bila kujali itikadi za vyama vyao wakapitisha sheria hii,”
alisema Dkt. Magufuli.
Aidha, Dkt. Magufuli amempongeza
Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete kwa kusaini sheria hiyo haraka mara
baada ya Bunge hilo kuipitisha kwa sababu alijua madhara ya dawa za
kulevya katika nchi yetu.
Amefafanua kuwa sheria imeeleza
wazi katika kifungu cha 10 cha Sheria Na.5 ya mwaka 2015 kuwa jukumu la
kupambana na dawa za kulevya linasimamiwa na Serikali pekee yaani Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, Makamo wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na
Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya au mtu yoyote
atakayekuwa amepewa mamlaka ya kusimamia Serikali.
Kwa upande wake Waziri Mkuu, Mhe.
Kassim Majaliwa amesema kuwa Taifa limeendelea kushuhudia kizazi chetu
kikiendelea kudidimia kwa sababu ya matumizi ya dawa za kulevya na
Serikali kwa mipango yake imeendelea kukemea, kudhibiti na kuchukua
hatua mbalimbali dhidi ya wazalishaji, wasambazaji, wauzaji na watumiaji
wa dawa hizo.
“Jambo hili limeleta athari kubwa
sana kwani vijana wetu wengi wamepoteza uwezo wa kujisimamia katika
shughuli zao za maendeleo kwa sababu baada ya matumizi tumeona athari
kadhaa zikiwezo za kudhoofishwa kwa mwili, uwezo wa kutafakari pamoja na
kutoweka kwa uwezo wa kufanya kazi,”alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Waziri Mkuu Majaliwa ameongeza
kuwa Taifa hili la Watanzania kwa kiasi kikubwa linawategemea vijana
waweze kuleta msukumo wa maendeleo ndani ya nchi hivyo jambo hili
likiachiwa linaweza kuleta athari kubwa katika ukuaji wa uchumi na
maendeleo yetu kwa ujumla wake.
Alisisitiza kuwa vita hii
ilianza, inaendelea na itaendelea kupiganwa hadi imalizike hivyo
Watanzania hawana budi kuunga mkono jitihada zozote zinazofanywa na
Serikali kuhakikisha wanatokomeza uzalishaji, usambazaji, uuzaji na
matumizi yake kwa namna yoyote ile, kila mmoja anatakiwa kushiriki
kikamilifu ili kubaini matumizi ya dawa za kulevya ndani ya nchi hii.
No comments