TAHADHARI KWA WAMILIKI WA ARDHI WENYE MADENI YA PANGO LA ARDHI
Na Mboza Lwandiko
Lipa Kodi ya Ardhi kwa wakati,
uepuke kutozwa Tozo, Kutangazwa kwenye Vyombo vya Habari, Kupelekwa
Mahakamani na Kufutiwa umiliki wa ardhi yako, kwani Sheria ya Ardhi Na.
4 ya mwaka 1999 inaainisha gharama hizo kwa wasiozingatia ulipaji Kodi.
kutozingatia kulipa Kodi ya pango la Ardhi kwa wakati, ambapo mmiliki
asiyezingatia hilo kwanza; atatozwa Tozo na baadae Kupelekewa hati ya
madai na kufikishwa Mahakamani kulingana na kifungu Na. 50 na hatimaye
kufutiwa umiliki wa ardhi kulingana na Sheria hiyo hiyo katika kifungu
Na. 49-51.
Akizungumza na Waandishi wa
habari hivi karibuni wakati wa zoezi la kutoa notisi ya siku 14 kwa
wadaiwa sugu wa Kodi ya Pango la Ardhi. Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Dkt. Yamungu Kayandabila amesisitiza kwa
umma kuwa wadaiwa wote wa Pango la Ardhi wamekumbushwa na Serikali kwa
muda mrefu, na hivyo ni wakati wao kuhakikisha wanalipa madeni yao yote
ipaswavyo. Aliendelea kusema kuwa; kwa Mwaka wa fedha 2016/17 Wizara
imepanga kukusanya Sh. bilioni 111.77 kutokana na Kodi ya Pango la
Ardhi.
Dkt. Kayandabila alisema kwakuwa
Kodi ya Ardhi inatambulika bayana chini ya Sheria, kila mmiliki wa Ardhi
hana budi kuzingatia hilo. Malipo ya pango la ardhi yanatozwa kwa
wamiliki wa viwanja na mashamba yaliyopimwa na kumilikishwa kisheria.
Pia mtu yeyote anayemiliki ardhi iliyopimwa kisheria iwe imeendelezwa au
haijaendelezwa bado anapaswa kulipa kodi ya pango. Kila mmiliki
anaongozwa na mkataba wa kulipia kodi ya pango la ardhi kila mwaka
tarehe 1 (Mosi) Julai, Sheria ya Ardhi Na.4 ya mwaka 1999 kifungu cha
33 na kifungu kidogo cha 11 imetoa mwanya kwa walipa kodi kuendelea
kulipa bila adhabu hadi tarehe 31 Desemba ya mwaka unaohusika. Baada ya
hapo adhabu inatozwa. Mteja anapaswa kufanya malipo ya Kodi ya pango la
Ardhi kwa kuwa ananufaika na matumizi ya ardhi hiyo.
Vile vile, Mkuu wa Kitengo cha
Kodi katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Bwn. Dennis
Masami ameeleza kwa waandishi wa habari kuwa opereshini iliyoanza ya
kutoa notisi ya siku 14 kwa wadaiwa ni endelevu na kueleza kuwa hati za
madai zaidi ya 5000 zimeshasambazwa jijini Dar es Salaam. Alitaja
baadhi ya Kampuni ambazo zina madeni sugu ambazo zimepewa notisi ya siku
14 kulipa madeni ni pamoja na; Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uzalishaji
kwa Mauzo ya Nje (EPZA) anayedaiwa Shilingi milioni 144 na Mwananchi
Engineering wana deni la milioni 22. Kampuni nyingine ambazo zilipatiwa
notisi ni; Mohamed Interprise waliokuwa na deni la milioni 73 na
wameshalipa deni lote hivi karibuni na Lamada/Ilala – waliokuwa na deni
la milioni 54, wamepunguza deni kwa kulipa milioni 25.
Utaratibu wa ukadiriaji wa kodi
ya ardhi hufanyika kwa kuzingatia ukubwa wa ardhi inayomilikiwa na
thamani ya ardhi mahali ilipo (land value), vilevile kwa kuzingatia
huduma muhimu zilipo (miundombinu) na Matumizi ya ardhi husika kama vile
Biashara, viwanda, makazi, kilimo.
Aidha, Makadirio na malipo ya
kodi ya ardhi Kwa wamiliki wa ardhi yanafanyika katika maeneo
mbalimbali. Dar es Salaam; malipo ya kodi hufanyika Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi – Kivukoni, kwenye Kitengo cha Kodi na pia
kwenye Ofisi za Ardhi za Manispaa za Ilala, Kinondoni na Temeke. Katika
Mikoa; makadirio hufanywa kwenye Ofisi za Ardhi zinazotambulika za
Manispaa na Halmashauri za Miji na Wilayani kote nchini.
Aidha, Kumbukumbu za muhimu
zinahitajika wakati malipo yanapofanyika, kwa wale ambao kumbukumbu zao
za umiliki zilishaingizwa kwenye Kompyuta wanatakiwa wakumbuke namba ya
kumbukumbu ya kulipia yenye tarakimu sita (Lot Id Number). Hatahivyo,
wengine wote wanapaswa kufika katika maeneo yao ya kufanyia malipo na
risiti/ stakabadhi ya mwisho ya malipo na hati au barua ya toleo
(Original Letter of Offer).
Malipo ya kodi kwa toleo jipya la
Kiwanja (Letter of Offer) yanapaswa kulipwa ndani ya muda wa siku 30
kuanzia tarehe ya toleo, vinginevyo itachukuliwa kwamba kiwanja
kimekataliwa ambacho kilikuwa kimeshakabidhiwa kwa muhusika.
Katika Kampeni ya uhamasishaji
ulipaji Kodi ya Pango la Ardhi, katika eneo la Mbagala – Dar es Salaam,
zoezi lililofanywa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kwa
kushirikiana na Kitengo cha Kodi. Afisa Sheria; Seif Mahiza, aliyekuwa
akiongea na Wananchi wa Mbagala alisisitiza kuwa; “Mwananchi ataona
mzigo wa kulipa pango lake la Kodi ya Ardhi pale tu atakapoacha kulipa
kwa wakati na kuwa na malimbikizo, lakini Mwananchi akijitahidi kulipa
kodi yake ya pango la Ardhi kila mwaka kwa wakati hataona mzigo katika
kutimiza jukumu hilo”.
Malipo ya kodi ya Pango la Ardhi
ni ya manufaa kwa Mmiliki ili kumhakikishia miliki salama na uhalali wa
mali yake ambayo ina uwezo wa kuzalisha katika nyanja mbalimbali; mfano
katika kukopa, kuzalisha mazao, kukodisha n.k. Lakini pia Ardhi hiyo
hiyo hutumika kunufaisha Taifa kwa ujumla kwa Maendeleo ya nchi nzima.
“Lipa Kodi ya Pango la Ardhi kwa Maendeleo ya Taifa Letu”
No comments