SUMA JKT KUJENGA BANDARI KAVU RUVU
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Bandari Nchini (TPA), Deusdedit Kakoko (Wa pili kushoto) akitoa
maelezo kwa Waziri wa Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame
Mbarawa (Wa pili kulia) kabla ya kutiliana saini mkataba wa ujenzi wa
bandari kavu baina ya TPA na Shirika la uzalishaji Mali la Jeshi la
kujenga Taifa –SUMA JKT jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Bandari (TPA), Deusdedit Kakoko (Wa pili kushoto) na Mwanasheria
Mkuu wa Shirika la uzalishaji Mali Jeshi la kujenga Taifa –SUMA JKT,
Kanali John Mbungo, (Wa pili kulia), wakitiliana saini mkataba wa ujenzi
wa bandari kavu katika eneo la Kwala-Ruvu mkoani Pwani. Mkataba huo
umesainiwa leo jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Bandari (TPA), Eng. Deusdedit Kakoko (kushoto) na Mwanasheria Mkuu wa
Shirika la uzalishaji Mali Jeshi la kujenga Taifa –SUMA JKT Kanali John
Mbungo (Kulia) wakikabidhiana mikataba ya ujezi wa wa bandari kavu
katika eneo la Kwala-Ruvu mkoani Pwani. Katikati ni Waziri wa Ujenzi ,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akishuhudia makabidhiano
hayo.
Waziri wa Ujenzi , Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa(Katikati), akisisitiza jambo kwa
watendaji wa Mamlaka ya Bandari (TPA) mara baada ya kutiliana saini
mkataba wa ujenzi wa wa bandari kavu katika eneo la Kwala-Ruvu mkoani
Pwani.
Picha na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
…………..
Mamlaka ya Bandari nchini (TPA),
imetiliana saini Mkataba wa ujenzi wa Bandari Kavu na Shirika la
Uzalishaji mali la Jeshi la kujenga Taifa (Suma JKT), eneo la Kwala –
Ruvu mkoani Pwani.
Mkataba huo wa zaidi ya shilingi
bilioni 7.2 unaitaka Suma JKT kukamilisha bandari hiyo katika kipindi
cha wiki Tisa kuanzia sasa ambapo tayari eneo la Hekta 500 zimetengwa
kwa ajili ya ujenzi huo.
Akizungumza jijini Dar es salaam
leo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa
amesema ujenzi huo utapunguza msongamano bandarini na katika jiji la Dar
es salaam kwa kuwa magari mengi ya mizigo yanayokuja bandarini kuchukua
mizigo sasa yataishia katika bandari hiyo.
“Mizigo itasafirishwa kwa njia ya
reli kutoka bandarini kwenda Ruvu, hivyo magari ya mizigo hayatafika Dar
es salaam na hivyo kupunguza msongamano”, amesema Waziri Mbarawa.
Aidha, Profesa Mbarawa ameitaka
Suma JKT kufanya kazi kwa uadilifu na kwa muda mfupi ili kuiwezesha
mipango na mikakati ya Mamlaka hiyo kufanikiwa kwa urahisi.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mbarawa amesema Mamlaka hiyo itaanza ujenzi wa gati lenye urefu wa mita
300 katika bandari za Dar es salaam na Mtwara ili kuwezesha meli kubwa
kuweza kutia nanga na kuongeza ufanisi wa Bandari nchini.
“Upanuzi wa Bandari za Dar es
salaam na Mtwara utavutia wasafirishaji wengi kutumia bandari hizi,
hivyo wafanyakazi wote wa Mamlaka hii wafanye kazi kwa bidii na weledi”,
amesisistiza Waziri Mbarawa.
Kwa upande wake Mwanasheria mkuu
wa JKT, Kanali John Mbungo, amemhakikishia Waziri huyo kuwa kazi ya
ujenzi huo itafanyika kwa ubora na katika kipindi kilichopangwa.
Ujenzi wa Bandari Kavu katika eneo la Ruvu ni mkakati wa Serikali wa kupunguza msongamano katika jiji la Dar es salaam.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments