Serikali yatoa msimamo katika kulinda kazi za filamu nchini
Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye (kushoto) akizungumza na wadau
wa sekta ya filamu (hawapo pichani) wakati wa kikao cha wadau
kuzungumzia sera ya filamu leo Jijini Dar es Salaam. Katikati ni Naibu
Waziri Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Annastazia Wambura na
Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bibi. Nuru Millao
…………………………………………………..
Na Lorietha Laurence – WHUSM
Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye ameeleza msimamo wa serikali
katika kulinda kazi za filamu zinazouzwa nchini kuzingatia sheria na. 4
ya mwaka 1976 ya utengenezaji wa filamu na Michezo ya kuigiza.
Mhe. Nnauye ameyasema hayo leo
Jijini Dar es Salaam alipokutana na wadau wa filamu ikiwa ni mwendelezo
wa Kipindi cha “Wadau Tuzungumze” kilichoandaliwa na Wizara kwa
kuwashirikisha wadau wake wa kisekta.
“Ni wajibu kwa wanatasnia wa
filamu kufuata sheria katika kuuza bidhaa zao bila kujali zimetoka nje
ya nchi au ni za hapa hapa nchini ili kuwa na soko huru na la haki kwa
filamu na michezo ya kuigiza” alisema Mhe. Nape.
Pamoja na hayo Mhe. Nnauye
aliongeza kuwa ni wajibu wa kila mwanatasnia wa filamu kuhakikisha kuwa
wanatoa ushirikiano katika kutoa maoni ya kuandaa Sera ya filamu ambayo
itakuwa mwongozo katika kuendesha na kusimamia kazi za filamu nchini.
Aidha Waziri Nape aliutaka
uongozi wa Wizara kwa kushirikiana na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu
kuhakikisha kuwa wanakutana na wadau ili kukamilisha uundwaji wa sera
hiyo.
“ Naomba Katibu Mkuu na Katibu
Mtendaji wa Bodi ya Filamu kuhakikisha kuwa mnawasikiliza wadau wa
filamu katika kuandaa sera hii na ningependa ikamilike mapema mwezi
wanne mwaka huu ili kuharakisha mchakato wa kulinda kazi kama ilivyokuwa
maadhimio ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli” alisema Mhe. Nnauye.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji
wa Bodi ya Filamu nchini Bibi. Joyce Fissoo aliahidi kutekeleza agizo na
kupanga kukutana na wadau wa filamu upande wa watayarishaji Februari 28
mwaka huu, ili kupata maoni kuhusu uundwaji wa sera ya filamu.
Naye Msanii wa Filamu za kuigiza
nchini Bw. Single Mtambalike amewataka wadau wa filamu kushirikiana na
serikali kwa kutoa maoni yao yatakayosaidia katika kukamilisha Sera ya
filamu itakayotoa mwongozo thabiti kwa tasnia hiyo.
Kipindi cha “Wadau Tuzungumze”
kimekuwa kikitoa fursa kwa wadau wa sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo kujadili mambo mbalimbali yanayohusu sekta hizo ikiwemo kutatua
changamoto zinazowakabili lengo ikiwa ni kuimarisha uhusiano mzuri
baina ya Wizara na wadau hao.
No comments