SABA WAFARIKI DUNIA KWA KUSOMBWA NA MAJI, RPC ATOA TAHADHARI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Naibu Kamishna Charles Mkumbo
Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi
la Polisi mkoani hapa limewataka wananchi kuwa makini na kuchukua
tahadhari zote katika kipindi hiki cha Masika. Akizungumza na waandishi
wa habari mchana wa leo ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha
Naibu Kamishna Charles Omari Mkumbo alisema katika kipindi hiki cha mvua
wananchi hawatakiwi kuvuka mito na mabonde yenye maji kwa hisia badala
yake wanatakiwa wawe na subira.
“Natoa
wito kwa wananchi wa mkoa wa Arusha katika kipindi hiki cha masika
hamtakiwi kujipa ujasiri na kuyakadiria maji ya mvua hivyo zinahitajika
tahadhari za kutosha dhidi ya watoto, au vyombo vyovyote vya usafiri kwani
maji hayo huwa yanakwenda kwa kasi, yasubirini yapite acheni hisia ili
kuhakikisha maisha yenu hayahatarishwi na mvua”. Alisisitiza Kamanda
Mkumbo.
Kamanda
Mkumbo alitoa wito huo baada ya jana usiku kunyesha mvua kubwa katika
maeneo mbalimbali ya mkoa huu na kusababisha vifo vya watu saba. Alisema
katika tukio la kwanza jana Usiku wa saa 4:00 katika kijiji cha Kimbolo
kata ya Enaboishu wilayani Arumeru, watu watano wote wakazi wa kijiji
cha Kyoga walifariki dunia baada ya gari aina ya Toyota Premio lenye
namba za usajili T 579 BSG kusombwa na maji.
Akiwataja
watu hao waliofariki katika tukio hilo kuwa ni Shengai Saiguran (30),
Nembris Mungaya (20), Minis Loyi (25), Inoti George (40) na Ngaisi Moluo
ambaye umri wake bado haujafahamika mara moja huku dereva wa gari hilo
Yusuph Jacobo akinusurika.
Kamanda
Mkumbo alisema mbali na vifo vya watu hao pia watu wengine wawili
walifariki dunia katika maeneo tofauti ambapo katika kijiji cha Keriani
mtu aitwaye Babu Robikeki alisombwa na maji kisha kufariki dunia wakati
anavuka mto wakati akitokea matembezini.
Wakati
mtu wa saba ni Seuli Meseyeki (37) dereva wa boda boda ambaye alikuwa
anaendesha pikipiki aina ya T-Better yenye namba za usajili T. 726 DFD
naye alisombwa na maji eneo la Olorieni Ngaramtoni wakati anavuka
barabara. Pia pikipiki aina ya Boxer yenye namba za usajili MC 892 ACR
iliokotwa maeneo ya Olasiti kwa Mawala halmashauri ya jiji la Arusha
huku dereva wake hajulikani alipo.
No comments