RAIS HAJATANGAZA KUFUTWA KWA VYAMA VYA UPINZANI- MAJALIWA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa
Rais, Dkt. John Magufuli hajawahi kutangaza ama kutoa kauli ya kufutwa kwa
vyama vya siasa nchini.
Ametoa kauli hiyo leo (Februari, 2, 2017) Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Mbowe katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu.
Katika swali lake Mheshimiwa Mbowe alisema Rais Dkt. Magufuli alinukuliwa akisema atahakikisha anafuta vyama vyama vya upinzani na ifikapo mwaka 2020 hakuna upinzani nchini.
Pia Mheshimiwa Mbowe alitaka kujua
nini kauli ya Serikali kuhusu kunyimwa dhamana kwa Mbunge wa Arusha Mjini, Mheshimiwa
Godbless Lema ambaye anashikiliwa kwa muda miezi mitatu.
Mbali na Mheshimiwa Lema, pia kiongozi
huyo alitaka kujua kuhusiana na kufungwa kwa Mbunge wa Kilombelo, Mheshimiwa Peter
Lijualikali pamoja na madiwani sita wa chama hicho ambao wamefungwa na viongozi
wengine 215 wanakabiliwa na kesi mbalimbali.
“Kwanza nataka nikanushe kwamba Mheshimiwa
Rais hajawahi kutangaza kuvifuta vyama vya upinzani. Pia Watanzania wote
wanajua nchi hii inaongozwa kwa sheria, kanuni na taratibu i,” amesema Waziri
Mkuu.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa “tunajua
katika kuendesha nchi tunaendesha kwa mihimili mitatu ipo Serikali, Mahakama na
Bunge na hakuna mhimili unaoweza kuuingilia mhimili mwingine,”.
“Pia Watanzania
wote wanajua kwamba jambo lolote ambalo lipo Mahakamani haliwezi kuzungumzwa mahali
pengine popote, hivyo siwezi kutumia nafasi hii kuzungumzia mambo yote yanayoendelea
chini ya sheria na yaliyo mahakamani,” amesema.
Wakati huo huo; Waziri Mkuu
amewahakikishia Watanzania kwamba suala la upungufu wa sukari halitatokea nchini kwa sababu viwanda vya ndani vinaendelea
kuzalisha na hadi mwishoni mwa Januari vilifikia asilimia 86 ya uzalishaji.
“Hadi kufikia mwishoni mwa msimu wa
uzalishaji ambao ni mwezi Machi, tunaweza kuwa tumefikia malengo na kama itajitokeza
upungufu Serikali itatafuta namna nzuri ya kupata sukari kwa kushirikiana na wenye
viwanda nchini,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo wakati
akijibu swali la Mbunge wa Mvomero, Mheshimiwa Suleiman Sadiq aliyetaka kujua
hali ya sukari ilivyo nchini kwa sasa na hatua gani zinazochukuliwa na Serikali
ili kunusuru hali ya uhaba wa sukari isijitokeze.
IMETOLEWA
NA:
OFISI YA
WAZIRI MKUU
S. L. P.
980,
DODOMA.
ALHAMIS,
FEBRUARI 02, 2017
No comments