Mwakyembe atembelewa na Uongozi wa TLS
Serikali imekiasa Chama cha
Wanasheria cha Tanganyika (TLS) kibaki kuwa chombo cha kitaaluma cha
kulinda weledi, viwango na maslahi mapana ya uanasheria na kisikubali
kuyumbishwa na mihemko ya uanaharakati wa kisiasa isiyo na tija
kitaaluma.
Akiongea na ujumbe wa TLS kwenye ofisi yake ndogo ya Dar es
Salaam leo (15/2/17), Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria, Dk.
Harrison Mwakyembe amesema TLS ibakie njia kuu kama ilivyo kwa vyama
vingine vya kitaaluma nchini, isighilibiwe na michepuko.
Amesema uanzishaji na uendeshaji wa TLS kwa sheria ya Bunge
umesukumwa miaka yote na dhamira njema ya Serikali ya kutaka kuilinda na
kuilea taaluma ya uanasheria ili ikue na ijenge weledi stahili na hivyo
itoe mchango bora katika ujenzi na uendeshaji wa utawala wa sheria
nchini.
“Ikiwa TLS sasa inajiona imekua kiasi cha kutosha na sasa
inataka iingie kwenye majukumu ya ziada ya uanaharakati wa kisiasa,
Serikali haitasita kuifuta sheria iliyoanzisha TLS ili chama hicho
kijisajili chini ya Sheria ya Vyama kama NGOs zingine nchini au
ikiwezekana chini ya Sheria ya Vyama vya Siasa kama vyama vingine vya
siasa nchini”.
Ameongeza kusema harakati zinazoendelea ndani ya TLS zenye
mwelekeo wa kisiasa, zimeifanya ofisi yangu isimame kidogo kukamilisha
marekebisho kadhaa ya sheria ya TLS maana hatma ya TLS haieleweki, “it
remains in the balance”.
Awali, waziri huyo aliueleza ujumbe huo wa TLS ukiongozwa na
Mtendaji Mkuu wa TLS, Wakili Lameck Calleb, kuwa Serikali imefarijika
sana kwa ushirikiano mkubwa uliotolewa na chama hicho katika maandalizi
ya muswada wa sheria ya huduma ya msaada wa kisheria ambayo imepitishwa
na Bunge na sasa unasubiri saini ya Rais wa Nchi kuwa sheria.
Aliongeza kuwa Wizara inaitegemea sana ushirikiano wa TLS
hata katika utungaji wa Kanuni za sheria hiyo mpya, mchakato wake ambao
tayari umeanza.
No comments