MREMA AMSHUKURU RAIS MAGUFULI KWA MATIBABU NCHINI INDIA
Mwenyekiti
wa Bodi ya Parole ya Taifa, Dkt. Augustine Lyatonga Mrema (katikati)
akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati
akitangaza tarehe ya uzinduzi wa bodi mpya ya parole taifa Machi 3 na 4, 2017 mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kushoto ni Msaidizi
wake, Clemence Munisi na kulia ni mkewe Rose Mrema.
Baadhi
ya waandishi wa habari wakimsikiliza kwa makini Mwenyekiti wa Bodi ya
Parole ya Taifa, Augustine Mrema (mwenye kofia),
wakati akitangaza tarehe ya uzinduzi wa bodi mpya ya parole taifa Machi
3 na 4, 2017 mapema hii leo jijini Dar es Salaam. (Picha na Eliphace Marwa - Maelezo)
Na Eliphace Marwa -Maelezo
Mwenyekiti
wa Bodi ya Parole ya Taifa, Augustine Mrema amemshukuru
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli
kwa kufanikisha safari ya kwenda nchini India kwa ajili ya kufanyiwa
uchunguzi wa afya yake.
Dkt.
Mrema ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na
waaandishi wa habari kuhusu uteuzi uliofanywa na Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba kwa kuwateua wajumbe wawili
wa bodi hiyo.
“Nachukua
nafasi hii kumshukuru Rais Magufuli , Waziri Mkuu, Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi Wizara ya Afya na Ikulu, kwa kunipeleka nchini India
kufanyiwa uchunguzi wa afya yangu na kupatiwa matibabu na sasa afya
yangu imeimarika na niko tayari kutekeleza majukumu yangu”, alisema
Mrema.
Akizungumzia
uteuzi uliofanywa na Waziri Nchemba, Mrema amesema kuwa toka
alivyoteuliwa na Rais Magufuli kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole Taifa,
Bodi hiyo haikukaa vikao kutokana na baadhi ya wajumbe wa Bodi hiyo
kumaliza muda wao.
“Nilipoteuliwa
na Rais kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole Taifa, Bodi ilikuwa bado
haijakutana na kufanya vikao kwasababu kuna wajumbe walikuwa wamemaliza
muda wao na Waziri wa Mambo ya Ndani alikuwa bado hajateua wajumbe
wengine lakini kwa sasa amakwisha fanya kazi ya uteuzi”, alisema Dkt.
Mrema.
Mrema
aliwataja walioteuliwa kuwa wajumbe wa Bodi ya Parole Taifa ni pamoja na
Bwana Francis Kistola na Bwana John William Nyoka.
Aidha
Mrema amempongeza Waziri wa Mambo ya Ndani kwa kukamilisha kazi ya
uteuzi na amewapongeza wajumbe walioteuliwa na kuwakaribisha kwa mikono
miwili kwenye bodi hiyo na kuomba ushirikiano wao na uzoefu wao ili
kukamilisha majukumu ya bodi ya Parole.
Vilevile
Mrema amesema kuwa kikao cha kwanza cha bodi mpya ya parole kitafanyika
tarehe 3 na 4 Machi 2017 jijini Dar es Salaam na bodi hiyo mpya
itazinduliwa siku hiyo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu
Nchemba.
No comments