KAMPUNI YA MELI YARUDISHA HUDUMA ZAKE MWANZA – UKEREWE
Na Biseko Lisso Ibrahim WUUM (U)
Kampuni ya Huduma ya Meli (MSCL)
imesema meli yake ya MV Clarias itarejesha safari zake za kila siku
kutoka Bandari ya Mwanza kwenda visiwa vya Ukerewe baada ya ukarabati
mkubwa kukamilika mwishoni mwa wiki hii.
Akitoa taarifa kwa Katibu Mkuu wa
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), mara
baada ya kukagua meli hiyo Kaimu Mtendaji Mkuu wa MSCL, Bw. Eric Hamisi
amesema meli hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 295 kwa safari moja
ukarabati wake umefikia hatua za mwisho na umetumia fedha za ndani kiasi
cha shilingi milioni 20.
“Kwa muda mrefu meli zetu
zimesimama kutoa huduma kwa sababu ya kukosa fedha za ukarabati, hivyo
tumeweka mkakati wa muda mfupi ambapo tumeweza kukusanya fedha za madeni
na tumekuja na mkakati wakudhibiti mapato ili tuweze kujiengea uwezo na
kufanya ukarabati kwa meli ambazo zilikuwa zimaharibika na kukaa tu”,
amesema Hamis.
Ameongeza kuwa kwa sasa pamoja na
mpango wa ukarabati wa meli hizo Kampuni iko kwenye hatua za mwisho
kuboresha mifumo ya kukatisha tiketi za meli zake zote kutoka kwenye
njia ya kawaida na kwenda njia ya ya kielektorniki ili kudhibiti mianya
ya upotevu wa mapato.
“Kwa sasa tunakamilisha utaratibu
wa manunuzi ili kupata mzabuni atakayetupa huduma za ukatishaji wa
tiketi kwa njia ya kielektoroniki ili kuweza kudhibiti mapato
yanayopotea kwa kutumia njia za kawaida”, alisisitiza Bw. Hamis.
Bw. Hamis ametanabaisha kuwa hatua
za kumpata mzabuni wa kujenga meli mpya moja katika Ziwa Viktoria ipo
katika hatua za mwisho ambapo meli hiyo ikikamilika itarahisisha usafiri
katika maeneo ya Kanda ya Ziwa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa
Sekta ya Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho amesema kuwa Serikali kwa sasa
inashughulikia suala la mishahara ili kuimairisha utendaji wa kampuni
hiyo.
Aidha, amewataka kuhakikisha
wanadhibiti mianya yote ya mapato ili kuhakikisha Kampuni inatumia fedha
zake za ndani katika ukarabati wa meli zake.
Kampuni ya MSCL iko kwenye mpango
mkakati wa muda mfupi ambao unaishia mwezi Aprili mwaka huu ambapo
pamoja na kuboresha mifumo mbalimbali imejipanga kukarabati Meli nne
ambazo ni MV clarias, MV Serengeti, MT. Sangara na ML Wimbi.
No comments