KAMATI YA UTENDAJI YAMALIZA TOFAUTI ZAKE NA BARAZA LA WADHAMINI SIMBA
Mwenyekiti
wa Baraza La Wadhamini wa Simba Mzee Hamis Kilomoni (katikati) akiwa
ameshikana mikono na viongozi wa kamati ya utendaji wa Simba, Rais wa
Klabu ya Simba Evance Aveva, Mkuu wa kitengo wa habari na mawasiliano
Haji Manara, Mjumbe wa kamati ya utendaji na mwenyekiti wa kamati ya
usajili Zacharia Hanspope.
Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
Baraza
la Wadhamini wa Klabu ya Simba limekubali yaishe baada ya kukutana leo
na na Kamati ya utendaji ya Klabu hiyo na kuwataka wapeleke mpango kazi
wa mabadiliko ili kufikia maamuzi yatakayokuwa na manufaa ndani ya klabu
hiyo kongwe hapa nchini.
Mwenyekiti wa Baraza hilo, Mzee Hamis Kilomoni alisema wanatambua
kila binadamu anafanya makosa na kama mtu akifanya kosa hakuna budi
kumsamehe na kushirikiana kufanya mambo mbalimbali ambayo yataleta
maendeleo.
Alisema Kamati hiyo ilifanya vikao vyake na kugundua Uongozi wa
Simba kwa ujumla ulikosea kufanya maamuzi yake na kuamua kuwasamehe kwa
yote waliyoyakosea ili kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji
wa klabu hiyo kutoka kumilikiwa na wanachama na kuelekea kwa mwekezaji
mmoja. Ikumbukwe kuwa baraza hilo liligomea hatua za mabadiliko ya
uendeshaji wa klabu hiyo yaliyotangazwa kufanywa na kamati tendaji tangu
mwaka jana kwa madai ya kutotimiza matakwa mbalimbali ya kisheria
ikiwemo kupuuzia baraza hilo linalotambulika kisheria.
"Niwajulishe mashabiki wa Simba kwa ujumla kwamba sisi hatuna
ugomvi na Kamati tendaji ya Simba lakini kilichokuwa kikifanyika ni
kuwashtua watekeleze matakwa yale tuliyokuwa tukiwaeleza kwa muda mrefu
na wao walikuwa hawajayatekeleza kikubwa zaidi hakuna mtu anayekataa
mabadiliko na sisi kama bodi ya wadhamini ya Simba SC ambao tunapenda
kuona mafanikio ya klabu tumewaagiza hawa viongozi watuletee mpango kazi
ili tujue ni namna gani mabadiliko hayo yatakavyokuwa na msaada kwa
klabu kiujumla," alisema Kilomoni.
Kilomoni aliendelea kusisitiza kuwa licha ya kuwataka viongozi wa
klabu hiyo kupeleka mpango kazi ili wafanye mabadiliko, Viongozi hao
wanapaswa kutambua mali zilizopo katika klabu hiyo ni za Simba
hazitokwenda kwa yeyote badala yake zitaendelea kubaki chini ya baraza
la wadhamini kama ilivyokuwa kipindi chote na mali za klabu hiyo sio za
mchezo wa mpira wa miguu pekee bali zinauhusiano na michezo mingine
licha ya kuwa kwa sasa haipo katika klabu hiyo.
Wakati huo huo, Rais wa Klabu hiyo, Evans Aveva alisema kumekuwa
na taarifa za kutokuwepo kwa maelewano chanya kati ya Uongozi wa klabu
hiyo na baraza la wadhamini jambo ambalo limemsukuma na kujitokeza
kulizungumzia ili kuwajuza watanzania kwamba hakuna tatizo lolote.
Alisema kilichokuwa kikitokea katika klabu hiyo ni changamoto za
kufanya kazi kwa pamoja na sehemu zote zinazowakutanisha watu mbalimbali
kutokea kwa baadhi ya watu kukubali jambo fulani na wengine kutokubali
ni lakawaida na halishangazi sana kwa kuwa Simba sio ya kwanza kupitia
hilo.
Alisema uongozi wa Simba umekuwa ukifanya kazi kwa ushirikiano na
mamlaka zote zilizopo katika klabu hiyo ili kuhakikisha inapata
mafanikio yale waliyoyapata kwa wakati waliojipangia na kuahidi kufanyia
kazi kwa wakati maelezo yaliyotolewa na baraza la wadhamini.
Rais wa Klabu ya Simba Evance Aveva akizungumza na waandishi wa
habari juu ya mustakabali wa uhalali wa Simba na bodi ya wadhamini na
kukubaliana kuweka wazi michakato yote ya mabadiliko ya klabu hiyo,
kulia ni Mwenyekiti wa Baraza La Wadhamini wa Simba Mzee Hamis Kilomoni.
Mwenyekiti wa Baraza La Wadhamini wa Simba Mzee Hamis Kilomoni
akizungumza na waandishi wa habari juu ya mustakabali wa uhalali wa
Simba na bodi ya wadhamini na kukubaliana kuweka wazi michakato yote ya
mabadiliko ya klabu hiyo.
No comments