HATUTAKUBALINA NA WACHOCHEZI – WAZIRI MKUU
*Asisitiza amani kwanza, masuala mengine baadaye
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali haitakubali kuona watu wachache wanachochea vurugu na
kusababisha watu wengine wapoteze maisha ilhali wao hawadhuriki.
Ametoa kauli hiyo jana jioni
(Jumatano, Februari 15, 2017) wakati akizungumza na maelfu ya wananchi
waliohudhuria mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa michezo wa mjini
Kibaya, wilayani Kiteto, mkoani Manyara.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika
siku ya kwanza ya ziara yake ya siku sita mkoani Manyara, alisema:
“Hatutakubaliana na wachochezi. Hatutakubaliana na yeyote
atakayesababisha kifo. Tukibaini kuna uchochezi, tutawasaka wahusika na
kuwashughulikia,” alisema.
“Hapa kulikuwa na majina ya
ajabuajabu, hatutakubali Kiteto iitwe Soweto au Kossovo, hapa ni
Tanzania. Hatuwezi kuishi kwa kubaguana, ni lazima tuheshimu maamuzi ya
wazee wetu wa kimila ambao wamesimamia zoezi hili ili kurejesha amani ya
Kiteto,” alisema.
Alisema zamani Kiteto kulikuwa hakuna lugha ya amani lakini hali kwa sasa imebadilika na kuwa nzuri na akasisitiza kwamba hakuna kurudi nyuma.
Alisema anamshukuru Waziri Mkuu
mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda kuwa kufuatilia suala hilo na kuunda tume ya
kutafuta amani wilayani Kiteto. “Nilipoingia madarakani, nami nilianza
kufuatilia suala hilo ili nijue chanzo hasa ni nini. Nikabaini kuwa
mgogoro mzima umechangiwa na chokochoko tu za watu wachache,” alisema.
Mapema, viongozi wa kimila
walimkabidhi Waziri Mkuu rungu, jembe dogo na jani la mti wa asili
(Kimasai unaitwa elisibie) ikiwa ni ishara amani ya kukomesha mapigano
baina ya wafugaji na wakulima. Pia alishiriki dua ya kuombea amani
ambayo iliongozwa na viongozi wa dini.
Mzee Mbambile Oloi Kurkur (65)
ambaye amejiita ni msimamizi wa mila za Kimasai alisema Mungu yuko na
anaweza kusimamia na kudumisha amani ambayo wameiombea. Alisema Mungu
ameumba mti wa ajabu ambao haukauki kwa mwaka mzima na majani na hubaki
ya kijani hata wakati wa kiangazi kikali. “Jani hili tunakukabidhi ikiwa
ni ishara ya makubaliano yetu kuwa ya kudumu,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya
Baraza la Amani la Wilaya ya Kiteto, Mzee Abubakar Mrisho alisema kamati
hiyo iliundwa na wazee 70 ambao walipita katika tarafa saba za wilaya
hiyo na kutoa elimu kwa wakazi wa vijiji vyote 23 juu ya umuhimu wa
suala kudumisha amani.
Ili kuhitimisha kazi yao, Mzee
Mrisho alimweleza Waziri Mkuu kwamba jana asubuhi, waliwachagua wazee
kutoka makabila manne ya Wamasai, Wanguu, Wakamba na Wagogo ili
wawakilishe makabila yote ya wilaya hiyo kwenye tambiko la kuoza ardhi.
“Baada ya tambiko tulitoa tamko
la Baraza la Amani kwamba mauaji hapa Kiteto sasa basi.Yeyote atakayeona
anabanwa, Kiteto haina nafasi naye tena,” alisema.
Kwa upande wao, viongozi wa dini
walitumia mkutano huo wa Waziri Mkuu kuomba dua kwa ajili ya kuombea
amani, haki, vita dhidi ya rushwa, ufisadi na dawa za kulevya na pia
kuombea mvua ya kiasi na yenye kuleta neema.
Askofu Isaiah Chambala wa CCT
alimuomba Mumgu awashe moyo wa upendo, amani na udugu miongoni mwa
wakazi wa Kiteto, mkoa wa Manyara na Tanzania kwa ujumla.
Padre Filbert Moita wa Kanisa la
Roma aliombea kuwe na haki na amani kwa watu wote na Mungu awasaidie
watu wake ili waheshimiane kidugu katika wilaya hiyo na mkoa mzima.
Mwalimu Juma Hicha wa BAKWATA
mbali ya kuombea amani wilayani humo, aliwaombea viongozi wa kitaifa
wapewe hekima ya kuongoza nchi na Mungu awajalie nguvu ya kupambana na
ufisadi, dhuluma na dawa za kulevya na zaidi ya yote Mungu awatie nguvu
ya kuikamilisha vita hiyo.
Leo Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake katika wilaya ya Simanjiro.
No comments