DC MUWANGO AIAMURU HALMASHAURI YA WILAYA YA NACHINGWEA KUREJESHA MAENEO YA ARDHI YALIYOVAMIWA
Mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mhe Rukia Muwango akisisitiza umuhimu wa kufanya mazoezi
Mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mhe Rukia Muwango akionyesha mfano wa ufanayaji mazoezi
Mkuu wa wilaya ya Nachingwea ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa Wilaya hiyo Mhe Rukia Muwango akifanya mazoezi katika uzinduzi huo
Matembezi yakiendelea vyema
Na Mathias Canal, Lindi
Mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mhe Rukia Muwango ameitaka Halmashauri ya Wilaya hiyo irejeshe maeneo yote ya wazi yaliyo vamiwa na kutumika kinyume cha matumizi yaliyolengwa.
Dc Muwango ametoa agizo hilo mjini Nachingwea kwenye uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya kudhibiti magonjwa yasioambukiza na yanayoweza kuzuilika kupitia mazoezi na michezo.
Uzinduzi huo uliofanyika katika uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine ambapo Alisema kuwa yeye kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo anatambua na anazotaarifa za kutosha kuwa maeneo mengi ambayo yalitengwa kwa ajili michezo na shuguli nyingine za umma yamevamiwa na kubadilishwa matumizi.
Dc Muwango ameitaka halmashauri hiyo kurejesha haraka kutoka mikononi mwa wavamizi.
Katika hali inayoonesha kuwa mkuu huyo wa Wilaya amelivalia njuga suala hilo, ameitaka Halmashauri hiyo ipeleke na kumkabidhi mikakati na taarifa za utekelezaji wa agizo lake haraka iwezekanavyo.
Sambamba na agizo hilo Muwango ameitaka Halmashauri hiyo kutenga maeneo kwa ajili ya michezo.
Amebainisha kuwa bila kuwa na maeneo ya wazi itakuwa vigumu kufanikiwa kukuza michezo na kuibua vipaji mbalimbali vya wanamichezo.
Amemuagiza Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kuwaandikia wakuu wa shule za sekondari na walimu wakuu wa shule za msingi ili warejeshe mbio za mchakamchaka kwenye shule zao kwani shule nyingi wanafunzi hawakimbii mchakamchaka.
"Jambo ambalo ni muhimu kwa afya na akili za wanafunz ila walimu wawe na usimamizi mzuri ili wanafunzi wasiathiriwe katika masomo na usalama wao," Alisistiza Muwango.
Akizungumzia umuhimu wa michezo na mazoezi Dc Muwango alisema kuwa licha ya kuimarisha, umoja,undugu na mshikamano.
Lakini pia mazoezi na michezo ni kichocheo kikubwa cha maendeleo, utulivu na amani katika jamii.
Alibainisha kuwa chanzo cha baadhi ya migogoro katika baadhi ya jamii ni magonjwa ambayo yanaweza kuepukwa kwa kufanya mazoezi ambapo Hata hivyo jamii husika hazitambui jbo hilo Badala yake inayahusisha magonjwa hayo na sababu zisizo na msingi Ikiwa ni pamoja na Imani potofu, uchawi na ushirikina mambo ambayo hupelekea kunyoosheana vidole na kusababisha migogoro.
"Lakini mtu akiwa mgonjwa hawezi kufanya shuguli za kiuchumi na maendeleo yake mwenyewe, Taifa na hata wanaomuuguza hawawezi kufanya kazi ambazo zingewaletea maendeleo," Aliongeza Muwango.
Mkuu huyo wa Wilaya alitoa wito kwa wananchi wilayani humo kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi bila kujali rika Huku akiwaasa kuunda vikundi vya michezo na mazoezi Kwa sababu madhara ya kutofanya mazoezi ni makubwa ambapo sio rahisi kuyabaini haraka.
Uzinduzi huo ambao ni utekelezaji wa agizo la makamu wa Rais aliyetaka kuwe na kampeni ya kitaifa ya kudhibiti magonjwa yasioambukiza na yanayozuilika kupitia michezo uliandaliwa na ofisi ya mkuu huyo wa wilaya ya Nachingwea Ambapo michezo mbalimbali ilichezwa, sambamba na upimaji wa afya na uchangiaji damu kwa hiari.
No comments