TAARIFA YA UOKOZI WACHIMBAJI MADINI WALIOFUKIWA NA KIFUSI- GEITA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA NISHATI NA MADINI
ZOEZI LA UOKOAJI WACHIMBAJI 15 WALIOFUKIWA NA KIFUSI KATIKA MGODI WA DHAHABU GEITA LAKAMILIKA KWA MAFANIKIO
Wizara ya Nishati na Madini inapenda kuufahamisha umma kuwa, Zoezi la kuwaokoa wachimbaji 15 waliofukiwa na kifusi tarehe 26/01/2017 kwenye mgodi wa dhahabu eneo la kijiji cha Mawemeru, Nyarugusu Wilayani Geita limekamilika kwa mafanikio.
Ajali
ya kufukiwa wachimbaji hao iliyohusisha Watanzania 14 na raia 1 wa
China ilitokea kwenye leseni ya uchimbaji wa Kati wa madini ya dhahabu
yenye Namba ML 492/2013 inayomilikiwa na Bw. Ahmed Mubarak Adam.
Chanzo cha ajali hiyo ilikuwa ni kuanguka kwa shaft ya mgodi huo na kufukiwa na kifusi wakati wachimbaji hao wakifanya kazi mgodini chini ya ardhi.
Tukio
la uokoaji limefanikiwa leo tarehe 29/01/2017 ambapo wahanga hao
walianza kutolewa shimoni kuanzia saa 5 hadi saa 5:30 asubuhi wote 15
wakiwa hai ingawa walikuwa wamedhoofika kiafya. Aidha,
wachimbaji hao wamepewa huduma ya kwanza katika eneo la ajali na kisha
kukimbizwa Hospitali Teule ya Rufaa ya Geita. Hadi sasa wachimbaji hao
wapo Hospitali wakiendelea na matibabu kwa uchunguzi zaidi wa afya zao.
Juhudi za kuokoa wachimbaji hao ambazo
zilifanyika kwa kufukua kifusi katika eneo la ajali zilianza mara baada
ya tukio hilo kutokea. Uongozi wa Mkoa wa Geita ukiongozwa na Mkuu wa
Mkoa Meja. Jen.(Mst) Ezekiel E. Kyunga ulishirikiana na Wataalam wa
Wizara ya Nishati na Madini na Kampuni za Madini mbalimbali mkoani Geita
katika zoezi la ufukuaji kifusi ili kuokoa maisha ya wchimbaji hao.
Kampuni zilizoshiriki kwa kutoa mitambo na vifaa mbalimbali ni Kampuni ya Busolwa Mining Ltd; Kampuni ya Geita Gold Mine (GGM); Kampuni ya Nyarugusu Mining Ltd; Nsangano Mining Project; Metchell Tanzania Drilling; WAJA Hospital pamoja na wachimbaji wadogo wa Mkoa wa Geita wakiongozwa na Viongozi wa wachimbaji madini Wilaya, Mkoa na Taifa.
Akizungumza
mara baada ya kuokolewa wachimbaji hao, Naibu Waziri wa Nishati na
Madini, Dkt. Medard amewashukuru wadau wote walioshiriki kwa hali na
mali kufukua kifusi na hatimaye kufanikiwa kuwatoa wachimbaji chini ya
ardhi wakiwa hai.
Dkt.
Kalemani amewaomba Watanzania kuendelea na moyo huo pale majanga kama
haya yanapotokea. Aidha, Dkt. Kalemani ameagiza shughuli zifungwe kwa
muda wa siku tano kwenye mgodi uliopata ajali kuanzia tarehe 29/01/2017
ili kutoa nafasi kwa Kamishna wa Madini kufanya tathmini ya hali ya
usalama wa mgodi na kutoa maelekezo kabla ya shughuli kuanza.
Vilevile,
amewataka wachimbaji wawe watulivu katika kipindi ambacho tathmini ya
hali ya usalama wa mgodi inafanyika na kuagiza Uongozi wa Mkoa
kuhakikisha kuwa ulinzi unaimarishwa eneo la mgodi ili watu wasiweze
kuingia na kuhatarisha maisha yao.
Pia,
ameagiza ukaguzi wa kina ufanyike kwenye migodi mingine ya wachimbaji
wadogo na ya kati eneo la Nyarugusu na kwingineko nchini ili kuhakikisha
kuwa migodi inakuwa salama kwa wachimbaji wa migodi husika.
Imetolewa na;
KATIBU MKUU
WIZARA YA NISHATI NA MADINI
29/1/2017
No comments