HALMASHAURI ZIFANYE KAZI KWA WELEDI-MAJALIWA
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa |
*Azitaka zisiwe pango la wezi, wazembe
WAZIRI MKUU Kassm Majaliwa
amesema wakati umefika wa kuwa na watumishi wenye weledi wa kutosha
kwenye Halmashauri zote nchini na pia hazitakiwi kuwa pango la wezi,
wazembe au jalala la kutupa wabadhilifu walioshindikana kwingineko.
Aidha, Waziri Mkuu amesemma
Serikali za Mitaa na Halmashauri zote nchini zinatakiwa zianze
kujitathmini na kujipanga vizuri zaidi kuona ni kwa namna gani zitakuwa
chachu ya maendeleo ya viwanda vinavyotarajiwa.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
(Jumatatu, Januari 30, 2017) wakati akifungua Kikao cha Baraza la
Mashauriano (RCC) mkoani Dodoma. Amesema kikao ni chombo muhimu na
endapo kitatumika vizuri kitaweza kusaidia kusukuma maendeleo ya Mkoa na
kupunguza migogoro kwenye Halmashauri.
Amesema Serikali itaendelea
kuongeza kiwango cha ruzuku kwa Halmashauri zote nchini kwa kadiri uwezo
utakavyoruhusu na kusisitiza kwamba fedha hizo lazima zisimamiwe vizuri
na zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo inayowagusa wananchi.
“Endapo itabainika kwamba kuna
baadhi ya Sheria zinazokwamisha utendaji katika Mamlaka za Serikali za
Mitaa, hatutasita kuzifanyia mapitio na hatimaye kuzibadili ili ziendane
na azma yetu ya kutoa huduma bora kwa wananchi,” amesema.
Amesema Serikali ina maslahi
makubwa kwa Serikali za Mitaa, sio tu kwa kuwa ni Serikali kamili katika
ngazi hiyo, bali pia kutokana na ukweli kwamba kero nyingi za wananchi
ziko katika ngazi hiyo.
Waziri Mkuu amesema vyanzo vingi
vya mapato ya Serikali vinapatikana kwenye Halmashauri huku changamoto
kubwa ikiwa ni kulegalega kwa Halmashauri nyingi katika ukusanyaji wa
mapato ya kodi na yasiyo ya kodi jambo linalozorotesha utoaji wa huduma
kwa wananchi.
Hivyo Waziri Mkuu ametoa rai kwa
Halmashauri hizo kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi na kutatua kero
zao kikamilifu na kwa wakati pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapato
na kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato.
Pia zihakikishe malipo yote
yanafanyika kwa njia za kielektoniki na zihamasishe vijana na akina mama
wajiunge kwenye vikundi vya uzalishaji mali na kuwapatia stadi za kazi
na mikopo yenye masharti nafuu ili waweze kuwa chanzo cha mapato hapo
baadaye.
Amesema watendaji wa Halmashauri
wanatakiwa kujiepusha na vitendo vya rushwa na ubadhilifu wa mali za
umma na uzembe kazini na watakaobainika kufanya vitendo hivyo
wachukuliwe hatua kali za kisheria na kinidhamu.
“Someni taarifa ya CAG (Mkaguzi
na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali) na kutoa majibu ya kina ya namna
mtakavyodhibiti mianya ya rushwa na ubadhilifu kama ilivyoainishwa
kwenye ripoti hizo,” amesema.
Hata hivyo amesema kila
Halmashauri iandae mpango wa utekelezaji wa Ilani ya CCM kwenye maeneo
makubwa ya kipaumbele kama vile ujenzi wa miundombinu ya shule,
maboresho kwenye sekta ya afya (ujenzi wa hospitali, zahanati na vituo
vya afya).
“Endeleeni kuwa na mahusiano
mazuri miongoni mwenu, mfanye kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na
taratibu. Kila mmoja kwa nafasi aliyonayo atimize wajibu wake na
kuzingatia mipaka ya nafasi yake. Punguzeni migogoro, matusi, dharau,
bezo na vitisho. Mshirikiane na jamii ione mpo wamoja,” amesema.
No comments