Ziara ya Mhe. Salva Kiir, Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini Tarehe 15 Aprili 2016
Ziara ya Mhe. Salva Kiir, Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini Tarehe 15 Aprili 2016.
Mhe.
Salva Kiir Mayardit, Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini atafanya ziara ya
kikazi ya siku moja nchini Tanzania tarehe 15 Aprili 2016. Rais Kiir
anakuja nchini kusaini Mkataba wa kuwezesha Jamhuri ya Sudan Kusini kuwa
Mwanachama kamili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambapo tangazo
la kukubaliwa kuwa Mwanachama wa EAC lilitangazwa na Mwenyekiti wa
Jumuiya hiyo, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa EAC uliofanyika
jijini Arusha mwezi Machi 2016.
Rais
Kiir atawasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
saa 3:00 asubuhi na baadaye ataelekea Ikulu na kupokelewa na Mwenyeji
wake, Mhe. Rais John Pombe Joseph Magufuli. Baada ya hapo, Viongozi hao
watashiriki hafla ya uwekaji saini ya Mkataba huo iliyopangwa kuanza saa
5:00 asubuhi na kisha watapata fursa ya kutoa hotuba na kusaini
Communique.
Rais
wa Sudan Kusini atashiriki hafla ya chakula cha mchana kilichoandaliwa
kwa heshima yake na Mwenyeji wake kabla ya kuondoka nchini baada ya
hafla hiyo.
Sudan
Kusini ni nchi ya sita kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo
inaongeza fursa nyingi za kiuchumi ambazo zinaweza kuzifaidisha Nchi
Wanachama ikiwemo Tanzania, endapo mipango madhubuti itawekwa
kuzichangamkia. Fursa hizo ni pamoja na za kibiashara kwa kuwa bidhaa
nyingi zinazotumika Sudan Kusini zinaagizwa kutoka Nje ya nchi. Hivyo,
jamii ya wafanyabiashara wa Tanzania wanahimizwa kuchangamkia fursa
zinazopatikana nchini humo na ndani ya Jumuiya kwa ujumla.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,
Dar es Salaam, 14 Aprili, 2016
No comments