Header Ads

ad

Breaking News

Yondani atoa la moyoni




BEKI wa Yanga, Kelvin Yondani, ambaye kwa sasa ni majeruhi baada ya kuchezewa rafu mbaya na Haruna Moshi ‘Boban’ wa Simba, amewaponda wenzake wanaofanya mambo ya kijinga uwanjani kwa kutafuta sifa kutoka kwa mashabiki.

Yondani aliumizwa mguu wake wa kulia na Boban, wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baina ya timu hizo Jumatano iliyopita, hali iliyowafanya wapenzi wa soka nchini kupatwa na hofu juu ya beki huyo kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu.

Tayari daktari wa Yanga, Juma Sufiani, aliweka wazi kuwa, Yondani atakuwa nje ya uwanja kwa takribani wiki mbili.  

Kwa kufahamu jinsi baadhi ya wachezaji wanavyohatarisha maisha ya wenzao kisoka kwa kuwachezea rafu za kijinga, Yondani amewataka wachezaji kufuata sheria 17 za soka ili kuepuka kuingia katika migogoro na wenzao, ambayo haina maana.

Akizungumza na SuperStar akiwa nyumbani kwake Mbagala jijini Dar es Salaam, Yondani alisema kuwa, ni kwa kufanya hivyo, wachezaji wanaweza kujiepusha kukatiza ndoto za wenzao katika soka.
“Tuache kuwasikiliza mashabiki ili tuchezea mpira, kila mmoja amesajiliwa katika timu yake ili kucheza soka na si vinginevyo,” alisema beki huyo aliyetua Yanga msimu huu akitokea Simba.

Kauli hiyo ya Yondani, inakuja huku kukiwa na madai kuwa, Boban alimchezea rafu ile kwa makusudi ili kuidhoofisha Yanga, katika pambano hilo la watani wa jadi, madai ambayo hata hivyo, kiungo huyo wa Wekundu wa Msimbazi, ameyapinga, na kusisitiza kuwa, hakudhamiria kumuumiza ‘rafiki’ yake huyo.

Tayari Yondani amesema kuwa, amemsamehe Boban kutokana na rafu hiyo aliyomchezea akiamini ilikuwa ni sehemu ya mchezo.

No comments