Yanga yamshitaki Akrama TFF
UONGOZI wa klabu ya Yanga, umemlalamikia
mwamuzi wa mchezo wao dhidi ya Simba, Mathew Akrama, na kulitaka Shirikiso la
Soka Tanzania (TFF), kuipitia upya mechi hiyo iliyochezwa Oktoba 3, mwaka huu
kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ili waangalie madudu yaliyofanywa
na mwamuzi huyo.
Yanga wamemlalamikia mwamuzi Akrama na
wasaidizi wake, Samuel Mpenzu kutoka
Arusha na Ephrony Ndissa wa Dar es Salaa, kuwa walishindwa kutafsiri sheria 17
za soka.
Akizungumza jana katika makao makuu ya klabu
hiyo, mitaa ya Jangwani na Twiga, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Lawrence Mwalusako,
alisema mwamuzi huo alikuwa akipendelea sana upande mmoja, na kusababisha kutoa
maamuzi yasiyo sahihi.
Mwalusako alisema kuwa, hata katika utoaji wa
kadi kwa wachezaji, alikuwa akipendelea sana wachezaji wa Simba, kwani makosa aliyofanya
Haruna Moshi ‘Boban’, hayakustahili kupewa kadi ya njano.
“Mwamuzi aliipendelea sana Simba, ile mechi
kila mmoja aliiona na makosa yaliyofanywa na Boban, pia yalionekana dhahiri,
lakini mwamuzi akampa kadi ya njano,” alisema Mwalusako.
Alisema kuwa, TFF inapaswa kuiangalia mechi
ile upya na kuitolea maamuzi dhidi ya mwamuzi Akrama, kwa kile alichokifanya,
kwani kila aliyeishuhudia aliona makosa yaliyokuwa yakifanyika.
Alisema kuwa, mbali na mwamuzi huyo wa kati, hata
wasaidizi wake walikuwa wakitoa maamuzi ya kuiuufaisha upande mmoja.
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara
uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, timu hizo zilitoka sare
ya bao 1-1.
No comments