TENGA AZITAKA KAMATI ZA UCHAGUZI KUSIMAMIA KANUNI
Rais wa TFF, Leodegar Tenga |
Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amezitaka Kamati
za Uchaguzi kufanya kazi kwa kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF
ili kuwa na uchaguzi huru na wa haki.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari, Dar es Salaam leo, Rais Tenga amesema uongozi wa mpira
wa miguu unahitaji uamuzi mgumu, hivyo Kamati za Uchaguzi ambazo zimeundwa kwa
mujibu wa Katiba zinatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni na si kuangalia
sura za watu.
Amepongeza
kamati zilizosimamia uchaguzi kwa kufuata kanuni, na ingawa kila mtu ana haki
ya kuongoza, jambo lolote lazima liwe na kanuni, kwani hata kwenye mikutano ya
hadhara kuna kanuni.
“Huwezi
kufika kwenye mkutano wa hadhara na wewe unaanzisha mkutano wako. Lazima kanuni
ziheshimiwe ili kufanya uchaguzi uwe huru na wa haki. Nini kimetokea kwenye
maeneo ambayo kuna matatizo? Kila mwanachama wetu (mkoa/chama shiriki) ana
Kamati ya Uchaguzi ambayo imeundwa kwa mujibu wa kanuni.
“Zile
kamati hazitekelezi majukumu yake, unampitisha mtu unajua hana sifa unasema
acha akafie mbele (Kamati ya Uchaguzi ya TFF). Kanuni zinasema jaza fomu
mwenyewe, weka nakala za vyeti na si kwamba huyu tunamjua. Kanuni zinatakiwa
zifuatwe, ukienda kinyume unaondolewa,” amesema.
Amesisitiza
kamati zifanye kazi kwa kufuata kanuni ili kusaidia mpira wa miguu kwani
zimeundwa kihalali, kwa hiyo zisiogope kuengua hata walioziteua kama hawana
sifa.
Pia
Rais Tenga amezitaka Kamati za Utendaji na Sekretarieti kutoziingilia Kamati za
Uchaguzi katika mchakato wa uchaguzi, badala yake zinatakiwa kuziwezesha tu
(facilitation).
Amesema
baadhi ya wagombea nao ni tatizo kwani wanaingia kwenye uchaguzi bila kuzielewa
Katiba za vyama vyao na Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF, hivyo ni vizuri
wakazielewa kwanza.
Rais
Tenga amesema ni vizuri wanachama wote wakafanya uchaguzi kabla ya uchaguzi wa
TFF utakaofanyika Desemba mwaka huu ili wapate fursa ya kupiga kura kwenye
uchaguzi huo wa shirikisho.
Vilevile
amewataka wadau kujitokeza kwa wingi kuwania uongozi kwenye chaguzi za vyama
wanachama wa TFF, kwani mwitikio umeonekana kuwa mdogo kulinganisha na umaarufu
wa mchezo wenyewe.
Amepongeza
vyama vya mikoa ambavyo tayari vimefanya uchaguzi wao. Baadhi ya vyama hivyo ni
Arusha, Dodoma, Iringa, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro, Manyara, Mara, Morogoro,
Mtwara na Singida.
No comments