Simba yabanwa na Kagera Sugar U/Taifa, zatoka 2-2
![]() |
Kikosi cha Simba |
KWELI Kagera Sugar ni kiboko ya vigogo! Mabingwa wa
soka nchini, Simba, jana walishindwa kutamba baada ya kubanwa na Wakata Miwa wa
Kagera, na kutoka nao sare ya mabao 2-2, katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja
wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo, Simba walianza kwa kasi na
kulisakama lango la wa Kagera Sugar, ambapo dakika ya nane, Felix Sunzu
akishindwa kuunganisha kwa kichwa mpira.
Dakika ya tisa, Sunzu alirekebisha makosa yake, kwa
kufunga bao kwa kichwa akiunganisha mpira uliopigwa na Mrisho Ngassa,
aliyewashinda ujanja mabeki wa Kagera Sugar.
Sunzu alikuwa akiisumbua ngome ya wapinzani wao, lakini
alishindwa kuiongezea bao timu yake ya Simba, baada ya kuunganisha kwa kichwa
mpira wa krosi uliotoka kwa Said Nassoro ‘Cholo’, na kutoka nje ya lango la
Kagera Sugar.
Kagera Sugar walizinduka na dakika ya 26, Daud
Jumanne, alishindwa kuunganisha vizuri mpira uliopigwa na George Kavila na
kutoka nje ya lango la Simba.
Simba walifanya shambulizi la nguvu dakika ya 29,
baada ya beki Juma Nyosso kuonana vizuri na Mwinyi Kazimoto, lakini mpira
aliopiga ulitoka nje ya lango la wapinzani wao.
Wakizidi kuliandamaa lango la wapinzani wao, Simba,
Ngassa na Haruna Moshi ‘Boban’, walipata nafasi nzuri, lakini walishindwa
kuifungia timu yao bao.
Pamoja na mashambulizi hayo, Kagera Sugar,
walijitutumua na kuliandama lango la wapinzani wao, ambapo dakika ya 43, Shija
Mkina, alikosa bao la wazi.
Ngassa aliwainua mashabiki wa Simba dakika ya 51,
baada ya kutumia vizuri makosa ya beki wa Kagera Sugar, Martin Muganyizi, bao
ambalo liliwafanya wachezaji wa Kagera kumfuata mwamuzi msaidizi namba moja,
Julius Kasitu kutoka Shinyanga aliyenyoosha juu kibendera, huku mwamuzi wa kati
Ronald Swai kutoka Arusha, akishindwa kumwangalia.
Mbaya wa Yanga, Them Felix, alithibitisha ubora wake
wa kuzifumania nyavu, baada ya kuifungia timu yake ya Kagera Sugar bao dakika
ya 65, kwa kichwa.
Wakiwa na nguvu mpya, Kagera Sugar walilisakama
lango la Simba na kufanikiwa kupata penalti baada ya Nyosso kumchezea vibaya
Paul Ngwai, penalti iliyotumbukizwa wavuni na Salum Kanoni.
Felix aliingia uwanjani kuchukua nafasi ya Darlington
Enyima, dakika ya 53, lakini dakika mbili baadaye akamchunulia Juma Kaseja na
kumpeleka nyavuni kuokota mpira ukiwa tayari umezitikisa.
Simba:
Juma Kaseja, Said Nassoro ‘Cholo’, Amir Maftah,
Juma Nyoso, Pascal Ochieng, Mwinyi Kazimoto, Mrisho Ngassa, Amri Kiemba, Felix Sunzu,
Haruna Moshi ‘Boban’, Emmanuel Okwi.
Kagera: Andrew Ntalla, Salum Kanoni, Martin Muganyizi,
Amandus Nesta, Benjamin Effe, Malagesi Mwangwa, Daud Jumanne, George Kavilla,
Shija Mkina, Darlington Enyima, Wilfred Ammeh.
Katika mechi ya utangulizi, Simba B iliichapa Ruvu
B, mabao 3-0, katika mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Simba B yalifungwa na Ramadhan Salum dakika
ya 65 na 70, ambapo bao la tatu likipachikwa wavuni na Miraj Athuman dakika ya
85.
No comments