Header Ads

ad

Breaking News

Si Simba, wala Yanga



 KAPSHENI: Mshambuliaji wa Yanga, Jerryson Tegete (kushoto), akiteta jambo na nahodha wa Simba, Juma Kaseja.

WAKONGWE wa soka hapa nchini timu za Simba na Yanga, zilitoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo ulikuwa wa kuvutia kwa muda wote, hivyo kutoa bonge la burudani kwa mashabiki wa soka waliofurika kwenye uwanja huo.

Simba ndio walikuwa wa kwanza kupachika bao lililofungwa na Amri Kiemba katika dakika ya tatu ya mchezi huo.
Kiemba alifunga bao hilo, akiunganisha krosi safi iliyopigwa na kiungo Mwinyi Kazimoto kutoka wingi ya kulia.

Mabeki wa Yanga walikosa umakini wa kuuzuia mpira huo, ambao ulikwenda moja kwa moja kwa Kiemba na kumchambua kipa Yaw Berko aliyechupa kuuokoa bila mafanikio.

Baada ya bao hilo la mapema, Simba walioneka kutawala mchezo ambapo sehemu ya kiungo iliyoongozwa na Jonas Mkude na Kiemba, iliweza kuzima moto wa Haruna Niyonzima na Athumani Iddi ‘Chuji’ wa Yanga.
Kutokana na Simba kuendelea kutawala safu ya kiungo, timu hiyo iliweza kupanga mashambulizi yake na kukosa bao dakika ya 12, baada ya shuti la Felix Sunzu kupaa juu ya lango la Yanga.
Yanga walionekana kubadilika na kushambulia kwa kushtukiza, ambapo dakika ya 16, shuti la Stephano Mwasyika lilipita pembeni kidogo ya mwamba na kutoka nje.

Mchezaji kiraka wa Simba, Shomari Kapombe alishirikiana vizuri na Juma Nyoso katika safu ya ulinzi, kuwadhibiti washambuliaji wa Yanga, Said Bahanunzi, Hamis Kiiza na Didier Kavumbagu.
Katika dakika ya 33, shuti la Mbuyi Twite wa Yanga liligonga mwamba waa juu na kutoka nje.

Kwa upande wake, Kiiza alishindwa kabisa kuonyesha cheche zake na hivyo kutolewa katika dakika ya 37 na nafasi yake kuchukuliwa na Frank Damayo.

Baada ya mapumziko, Yanga walianza kwa kufanya mabadiliko ambaapo Nizar Khalfani alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Kavumbagu.
Kuingia kwa Kavumbagu kwa upande wa Yanga kulionekana kuipa uhai kwa timu hiyo ambapo alishirikiana vyema na Bahanunzi katika kulitia mshikemshike lango la Simba.

Kuingia kwa Kavumbagu, kuliubadilisha mchezo huo ambapo safu ya ulinzi ya Simba ilikuwa na kazi ya ziada kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya Yanga.

Dakika ya 55, Kavumbagu alitikisa nyavu za Simba, lakini mwamuzi wa kati, Mathew Akrama alidai kuwa kabla nyota huyo kutoka Burundi kuukwamisha mpira huo nyavuni, alimchezea vibaya kipa wa Simba, Juma Kaseja.

Yanga waliandika bao la kusawazisha dakika ya 64 kwa mkwaju wa penalti iliyopigwa na Bahanunzi, baada ya Nyosso kuunawa mpira uliorushwa na Twite katika eneo la hatari.

Katika kipindi hicho cha pili, Yanga walionekana kung’ara sehemu ya kiungo jambo ambalo lilimlazimu kocha wa Simba, Milovan Cirkovic kumtoa Mkude na kumwingiza Haruna Moshi ‘Boban’, dakika ya 69.

Kutokana na mchezo huo kutawaliwa na ubabe wa hapa na pale, Simon Msuva alionyeshwa kadi nyekundu baada ya kumchezea vibaya Nyosso dakika ya 77.

Zikiwa zimesalia dakika za lala salama, Boban alimchezea vibaya beki wa Yanga, Kelvin Yondani na hivyo mchezaji huyo kutolewa na kushindwa kuendelea.

Kutokana na rafu hiyo, Boban alionyeshwa kadi ya njano na mwamuzi Akrama.

No comments