Ngassa kuikosa Coastal Union
Mrisho Ngassa |
MABINGWA wa soka nchini, Simba,
wameondoka jana kwenda jijini Tanga kuumana na Coastal Union, bila ya kiungo
mshambuliaji wake mpya, Mrisho Ngassa.
Ngassa, ataikosa mechi hiyo baada ya
kuwa mgonjwa, hivyo atawakosa Wagosi wa Kaya, watakaocheza nao Jumamosi kwenye
Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.
Akizungumza na gazeti hili jana,
Ofisa Habari wa klabu ya Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kuwa, Ngassa ni
miongoni mwa wachezaji wengine sita walioachwa katika msafari wa kwenda Tanga.
Aliwataja
wengini walioachwa ni kiungo Kiggi Makassy, Waziri Hamad, Haruna Shamte,
Ramadha Chombo ‘Redondo’, na Emmanuel Okwi, aliyekwenda nchini Uganda kuungana
na wenzake katika kikosi cha timu ya taifa ‘The Cranes’
Kamwaga alisema kwamba, kuhusu Ngassa,
ametemwa kwani bado hajapona malaria, ambayo ilimnyima nafasi ya kucheza dhidi JKT
Oljoro ya Arusha, mechi iliyopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na
kuibuka na ushindi wa mabao 4-1.
Ofisa habari huyo alisema kwa upande
wa Makassy, aliumia katika mechi ya kirafiki iliyochezwa juzi kwenye dhidi ya
Azam FC uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex. Simba ilishinda mabao 3-2.
Kamwaga alimtaja mchezaji mwingine
anayesumbuliwa na malaria ambaye hakuwemo kwenye msafara huo ni Redondo, wakati
Shamte, Waziri na Koman Billi Keita, ni majeruhi.
“Tunakwenda tukiwa na nguvu, na kila
mchezaji anaamini kuwa, tutaibuka na ushindi dhidi ya Coastal Union,” alisema
Kamwaga.
Kamwaga alisema kuwa, Simba
imekamilika kila idara, hivyto kukosekana kwa wachezaji hao, hakutakuwa na
pengo lolote, kwani wapo watakaofanya kazi vizuri ya kuwapa raha mashabiki wa
timu hiyo.
Simba, inaongoza Ligi Kuu Bara kwa
kushinda mechi tano na kutoka sare moja, ikijikusanyia pointi 16, hivyo
wataingia uwanjani kutaka kuendeleza rekodi yao ya ushindi, huku Coastal Union
wakiwa chini ya kocha Hemed Morocco, wakitaka kulinda heshima ya nyumbani.
No comments