Header Ads

ad

Breaking News

Coastal yaisimamisha Simba Mkwakwani


Kikosi cha Simba


Na Abdallah Mkwinda, Tanga

MABINGWA wa soka nchini, Simba, leo walibanwa mbavu na Wagosi wa Kaya, Coastal Union, katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.

Simba walianza mchezo kwa kulisakama lango la Coastal Union, ambapo dakika ya sita, kipa Jackson Chove, alifanya kazi kubwa ya kuuwahi mpira na kumzidi ujanja beki Amir Maftah na kuuondosha katika eneo lake la hatari.

Coastal Union walijibu shambulizi hilo, ambapo dakika ya nane, Seleman Selembe, alipokea pasi nzuri kutoka kwa Razack Halfan na kupiga shuti kali lililopaa juu ya lango la Simba.

Wakicheza mbele ya mashabiki wao, Coastal Union walipata nafasi nyingine dakika ya 10, Jamal Machelanga, alishindwa kuipatia bao timu yake baada ya kushuti lake kali kupiga nje kidogo ya lango la Simba, huku kipa Juma Kaseja akiruka bila mafanikio.

Haruna Chanogo wa Simba, alifanikiwa kumpita beki Said Sued na kupiga shuti kali lililogonga mwamba wa juu wa lango la Simba.
Dakika ya 35, Nassoro Masoud ‘Cholo’ alipiga krosi safi, lakini kipa Chove akiwa katikati ya washambuliaji wa Simba, aliudaka mpira huo.
Coastal Union walijibu shambulizi hilo dakika ya 39, lakini Nsa Job aliikosesha timu yake bao la wazi, baada ya kushindwa kutumia vizuri mpira wa krosi uliopigwa na Selembe, aliyemtoka beki Pascal Ochieng.
Kipindi cha pili timu zote ziliingia kwa kusaka bao la mapema, ambapo dakika ya 57, Atupele Green, alipiga shuti kali langoni mwa Simba, lakini lilitoka nje kidogo.
Dakika ya 63, Nsa Job, alipata nafasi nzuri na kupiga shuti kali lililopanguliwa na kipa Juma Kaseja, ambapo Maftah aliuondosha mpira huo katika eneo lao la hatari.
Coastal Union ilipata pigo dakika ya 69, baada ya Job kutolewa nje kwa kadi nyekundu iliyotoewa na mwamuzi Simon Mbelwa wa Pwani, akioneshwa kadi ya pili ya njano, kwa kumchezea vibaya, Ochieng wa Simba.
Haruna Moshi ‘Boban’, alishindwa kutumia vizuri nafasi aliyopata dakika ya 78, baada ya mpira aliopiga kutoka nje ya lango la Coastal Union.
Coastal: Jackson Chove, Said Sued, Juma Jabu, Mbwana Hamis, Jamal Machelenga/Ismail Hamis, Jerry Santo, Mohamed Athuman/Daniel Lyanga, Seleman Selembe, Atupele Green, Nsa Job, Razack Khalfan/Lameck Mbonde
Simba: Juma Kaseja, Nassoro Masoud ‘Cholo’, Amir Maftah, Pascal Ochieng, Shomari Kapombe, Miwnyi Kazimoto, Amri Kiemba, Felix Sunzu, Daniel Akuffor/Salum Kinje, Haruna Chanogo/Uhuru Seleman.

ciao

No comments