Yanga yaua Taifa, yaichapa JKT Ruvu 4-1
Na Mwandishi Wetuu
YANGA jana ilizinduka katika Ligi
Kuu Tanzania Bara baada ya kuichapa JKT Ruvu mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam.
Katika mechi ya kwanza ya ligi hiyo,
mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati waliambulia suluhu ugenini dhidi ya
Prisons Mbeya, kabla ya kulala kwa mabao 3-0 dhidi ya Mtibwa Sugar mjini
Morogoro katikati ya wiki.
Na ikicheza bila Kocha Mkuu, Tom
Saintfiet aliyetimuliwa juzi, Yanga iliuanza mchezo huo wa jana kwa kasi ya
ajabu na kufanikiwa kupata bao la kwanza dakika ya tano kupitia kwa nahodha
wake, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, akipokea krosi ya Athuman Idd ‘Chuji’,
aliyepokea mpira wa adhabu kutoka kwa Haruna Niyonzima.
Adhabu hiyo ilitokan na Simon Msuva
kuangushwa na Damas Makwaya nje kidogo ya eneo la hatari.
Bao la pili la Yanga lilifungwa na
Didier Kavumbagu katika dakika ya 32 kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na beki
wa kushoto Oscar Joshua.
Katika kipindi cha pili, Yanga
waliendeleza kasi yao na kupata bao la tatu kupitia kwa Msuva kutokana na
uzembe wa mabeki wa JKT Ruvu kushindwa kuondoa mpira katika eneo la hatari.
Kavumbagu alifunga hesabu ya mabao
ya Yanga baada ya kuifungia timu yake hiyo bao la nne kutokana na makosa ya
kipa wa JKT Ruvu ambaye aliutema mpira alioudaka kutokana na shuti kali la
Joshua.
JKT Ruvu walipata bao la kufutia
machozi kupitia kwa Credo Mwaipopo, ikiwa ni baada ya Joshua kufanya makosa yaliyotumiwa
vyema na Hussein Bunu aliyeinasa pasi ya kizembe ya beki huyo na kumpasia
mfungaji, hiyo ikiwa ni dakika ya 68.
Baada ya bao hilo, JKT Ruvu
walionekana kucharuka na kufanya mashambulizi ya nguvu langoni mwa Yanga,
lakini kipa wa timu hiyo, Yaw Berko, alikuwa imara kuokoa michomo yote
iliyoelekezwa langoni mwake.
Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo
uliochezwa kwenye Uwanja wa Chamazi, Azam iliichapa Mtibwa Sugar bao 1-0, bao
lililowekwa kimiani na Kipre Tchetche dakika ya 29.
No comments