Simba yaifundisha kazi TFF
Na Mwandishi Wetu
UONGOZI wa klabu Simba, umeitaka Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Soka (TFF),
kukutana haraka kujadili suala la mshambuliaji wao, Emmanuel Okwi, aliyepewa
kadi nyekundu katika mechi dhidi ya JKT Ruvu.
Mchezaji huyo wa kutegemewa wa klabu hiyo, alikumbana na adhabu hiyo, baada
ya kumpiga kiwiko beki wa JKT Ruvu, Kessy Mapande, ambapo Simba iliibuka na
ushindi wa mabao 2-0.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga, alisema kwa upande wao
wanaitaka kamati ya ligi kukutana haraka, ili kujua hatma ya mchezaji wao.
Lengo la Simba ni kujua mchezaji huyo kama atacheza katika mechi dhidi ya
watani wao, Yanga, ambayo inatarajiwa kupigwa Oktaba 3, mwaka huu kwenye Uwanja
wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, licha ya Simba kuishinikiza kamati ya ligi kukutana haraka,
lakini Kamwaga alikiri kuwa, kanuni zimewabana na hivyo wanataka kujua ripoti
ya mwamuzi iliwasilishwa TFF kwa lengo la kamati ya ligi kuijadili.
“Tunafahamu kuwa, kadi nyekundu ya moja kwa moja ni kukosa mechi tatu,
lakini inaweza kuwa mbili kulingana na ripoti ya mwamuzi, ambapo katika mechi
hiyo, alikuwa Andrew Shamba wa Dar es Salaam,” alisema Kamwaga.
Kamwaga alisema hofu yao inaweza kuwa ripoti inamtaka Okwi kukosa mechi
mbili, lakini kama kamati hiyo ya ligi haitakaa mapema, wanaweza kukosa haki
yao ya msingi.
Wakati Simba wakiwa na kigugumiza hicho, TFF hivi karibuni ilizitaka timu
za Ligi Kuu kuwa na utaratibu wa kuweka kumbukumbu ya matukio, ili kuepuka
migogoro ya mara kwa mara.
Hata hivyo, TFF imedai kuwa, milango ipo wazi kwa klabu ambazo zina mashaka
na kumbukumbuku zao, hivyo ni vema kwenda kuhakiki ili kujiridhisha.
No comments