Ngassa ni mwisho wa matatizo, apiga bao la ushindi Simba
MSHAMBULIAJI wa pembeni wa timu ya Simba, Mrisho Ngassa,
amezidi kuzitendea haki fedha za usajili zilizotolewa na klabu hiyo, kwa
kuonesha kiwango cha hali juu, huku akichangia sehemu kubwa ya ushindi wa timu
hiyo dhidi ya Tanzania Prisons wa mabao 2-1 .
Katika mechi zote alizocheza, Ngassa amekuwa chachu ya
ushindi kwa kufunga ama kutoa pasi za mwisho za mabao ya timu yake, ambapo jana
aliifungia timu yake bao la pili lililowapa ushindi katika mchezo huo uliopigwa
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika mechi ya leo, Ngassa alikuwa akiwasumbua mabeki wa
Prisons ya Mbeya, ambayo imerejea Ligi Kuu Bara, baada ya kushuka daraja miaka,
huku akitoa pasi za mwisho, ambapo mojawapo ikiwa kwa Ramadhan Chombo
‘Redondo’, aliyebaki na kipa David Abdallah, aliyeokoa kwa miguu.
Mbali na Ngassa, Prisons katika mchezo huo uliokuwa wa
kuvutia huku timu zote zikishambulia, ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya
sita, lililofungwa na Lugano Mwangama kwa shuti kali, aliloshindwa kudaka kipa
wa Simba, Juma Kaseja.
Kazi nzuri iliyofanywa na Mwinyi Kazimoto kumsukumia pasi
nzuri Amir Maftah, ilizaa bao baada ya beki huyo wa kushoto kutoa pasi safi
iliyomkuta Mzambia Felix Sunzu na kuisawazishia timu yake bao hilo.
Bao hilo liliwaongezea nguvu Simba, ambapo dakika ya
48, Sunzu alishindwa kuunganisha vizuri
kwa kichwa, mpira wa krosi uliopigwa na Ngassa na kutoka nje.
Ngassa akidhihirisha ubora wa kiwango chake, aliwainua
mashabiki wa Simba, baada ya kuifungia timu yake bao la pili dakika ya 55, kwa
shuti kali lililompita kipa Abdallah, aliyejaribu kuudaka na kushuhudia nyavu
zake zikitikisika.
Katika mchezo huo, beki wa kushoto wa Simba, Amir Maftah
alitolewa nje dakika ya 81, kwa kuonesha kadi nyekundu na mwamuzi Paul Soleji
kutoka Mwanza, baada ya kumchezea vibaya wa Khalid Fupi wa Tanzania Prisons.
Simba,
lkwa matokeo hayo imerejea kileleni mwa ligi hiyo, baada ya kushinda mechi zote
nne, ikiwa na pointi 12, ikifuatiwa na azam FC iliyojikusanyia pointi tisa,
huku Coastal Union wakiwa na pointi nane.
Simba:
Juma Kaseja, Nassoro Masoud ‘Cholo’, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Juma Nyosso,
Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba, Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Edward Christopher,
Felix Sunzu, Mrisho Ngassa.
Prisons:
David Abdallah, Aziz
Sibo, Laurian Mpalile, Lugano Mwangama, David Mwantika, Khalid Fupi, Misango
Magai, Fred Chudu, Elias Maguri, Peter Michael,John Matei.
No comments