KAMSHINA MMOJA AONDOLEWA KWENYE LIGI
Kamati
ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilikutana jana (Septemba
25 mwaka huu) kupitia ripoti za mechi 21 za Ligi Kuu ya Vodacom ambazo
zimeshachezwa mpaka sasa, na kuzifanyia uamuzi wa kikanuni ikiwemo kumuondoa
Kamishna mmoja.
George
Komba aliyekuwa Kamishna kwenye mechi namba 20 kati ya Simba na Ruvu Shooting
ameondolewa kwenye orodha ya makamishna wa ligi kutokana na upungufu
uliojitokeza katika ripoti yake.
Klabu
ambazo zimeandikwa barua za onyo ni African Lyon kwa kwenda uwanjani na jezi
tofauti na zile ilizoonesha kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi (pre match
meeting), Mtibwa Sugar kwa kuchelewa kuwasilisha leseni za wachezaji wake
wakati wa mechi na Ruvu Shooting kwa ushangiliaji uliopita kiasi kwenye mechi
yao dhidi ya Simba.
Kamati
pia imethibitisha kadi nyekundu ya Emmanuel Okwi kwa kumpiga kiwiko Kessy
Mapande wa JKT Ruvu, hivyo kwa mujibu wa Kanuni ya 25(1)() anakosa mechi tatu
na kulipa faini ya sh. 500,000. Mchezaji huyo atakosa mechi namba 20, 27 na 80.
Kwa
upande wa waamuzi, Ronald Swai ameandikiwa barua ya onyo kutokana na upungufu
alioonesha kwenye mechi kati ya Simba na Ruvu Shooting iliyochezwa Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Wamiliki
wa viwanja vya Mkwakwani, Tanga na Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya wameandikiwa
barua ya kuvifanyia marekebisho viwanja vyao katika maeneo mbalimbali yenye
upungufu ikiwemo uzio wa kutenganisha wachezaji na washabiki.
Mchezaji
Faustin Lukoo wa Polisi Moro ambaye kwa mujibu wa ripoti ya mwamuzi aliyemtoa
nje kwa kadi nyekundu alimtukana mchezaji mwenzake kwenye mechi dhidi ya
African Lyon na Katibu wa Oljoro JKT aliyemwaga maji kwenye chumba cha timu ya
Polisi Moro, masuala yao ni ya kinidhamu, hivyo yamepelekwa Kamati ya Nidhamu
na Usuluhishi kwa ajili ya hatua zaidi.
Kwa
klabu ambazo timu zao mpaka sasa zinacheza mechi bila kuwa na logo ya mdhamini,
suala hilo limepelekwa kwa wadhamini Vodacom kwa vile wenyewe ndiyo wanaogawa
vifaa hivyo.
No comments