Coastal yaichapa Kagera Sugar
Na Mwandishi Wetu, Tanga
TIMU ya Coastal Union ya jijini Tanga, jana
iliichapa Kagera Sugar mabao 3-2, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara
uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani, jana.
Katika mchezo huo uliokuwa wa kusisimua, Coastal
Union walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 38, lililowekwa kimiani na Daniel
Lyanga, baada ya kuunganisha mpira wa konauliopigwa na Said Sued.
Bao hilo liliwaongezea nguvu, ambapo dakika ya 40,
Nsa Job aliwainua mashabiki wa Coastal Union kwa kuifungia timu yake bao la
pili.
Dakika mbili baadaye, Kagera Sugar walijitutumua na
kufanikiwa kupata bao la kwanza kupitia kwa Amandus Nesta.
Nsa aliiongezea timu yake bao la tatu baada ya
kumtoka beki wa Kagera Sugar, Salum Kanon na kuukwamisha mpira kimiani.
Hata hivyo, Kagera Sugar hawakukata tama, waliongeza
mashambulizi na kufanikiwa kupata bao la pili lililofungwa kwa njia ya penalti,
baada ya Sued kumchezea vibaya mshambuliaji mmoja wa wapinzani, ambapo Kanon
aliifungia timu hiyo bao hilo.
No comments