Ngassa aigomea Azam
BAADA ya Simba na Yanga kuvutana juu ya mshambuliaji
wa Azam FC, Mrisho Nggasa, hatimaye jana ametua kwa Wekundu wa Msimbazi, Simba
SC, kwa mkopo.
Ngassa ambaye alionesha mapenzi ya wazi ya kutaka kwenda
Yanga, lakini uongozi wa Azam FC uliamua kutoa ofa kwa mchezaji huyo kwa timu
yoyote itakayokuwa ikimtaka.
Baada ya kutoa hofa hiyo, timu za Simba na Yanga
zilituma maombi katika timu yake ya Azam FC, lakini jana, Simba walifanikiwa
kumnasa kwa mkopo wa ada ya sh. milioni 25.
Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa wa Habari wa
Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kwamba,
wamefanikiwa kumnasa Nggasa kwa mkopo.
“Tayari tumemalizana na Azam FC, tumemchukua kwa
mkopo, tutamwangalia hadi Desemba mwaka huu, kama atafanya vizuri, tutamsajili
moja kwa moja kwa kutumia ada itakayolipwa na timu ambayo Emmanuel Okwi
anafanya majaribio,”,” alisema Kamwaga.
SuperStar ilimtafuta Meneja wa Azam FC, Patrick
Kahemele, ili kujua ukweli wa habari hizo, ambapo alikiri na kusema kuwa,
wamemtoa kwa mkopo Simba.
“Ni kweli tumemtoa kwa mkopo Simba, wametulipa sh. milioni 20, na watakuwa
wanamlipa mshahara wenyewe,” alisema.
Alipoulizwa kama mshambuliaji huyo alishirikishwa
kwenye vikao vyao vya kujadiliana uhamisho wake, alisema kuwa, hakushirikishwa,
lakini atapewa taarifa ya maandishi.
“Yeye ni mchezaji, tumeamua kumpeleka Simba bila ya
kumshirikisha, huu ni kama uhamisho kutoka kituo kimoja kwenda kingine,”
alisema.
“Ninapozungumza na wewe, tunamwandikia barua ya
kumweleza maamuzi yetu,” alisema.
Wakati huohuo, baba mzazi wa Mrisho, Khalfan Ngassa,
alisema kuwa, mtoto wake alimpigia simu ya kumtaka ushauri kuhusu uhamisho huo.
Mrisho alimweleza baba yake kuwa, amepata taarifa ya
ujumbe mfupi wa simu, kuwa amepelekwa Simba kwa mkopo bila ya kushirikishwa.
Baba yake alimuuliza kama alishirikishwa kwenye
mpango huo wa uhamisho, ambapo Mrisho alijibu kuwa, hakushirikishwa.
“Mimi nimeambiwa kwa ujumbe mfupi wa maneno kwenye
simu, sikushirikishwa katika suala hilo, lakini malengo yangu ni kurudi Yanga,”
alisema.
Baba yake alimtaka mtoto wake huyo kuendelea na
malengo yake, kwani tayari alikuwa na mtandao mkubwa wa marafiki ndani na nje
ya uwanja.
Mzee Ngassa alisema: “Nimemshauri kurejea katika
timu yake ya zamani ambayo amezoeana na kila mmoja mpaka viongozi, kama akienda
Simba ataanza kazi upya ya kujenga mahusiano ya ndani na nje ya uwanja,”
alisema.
No comments