Header Ads

ad

Breaking News

Yondani halali Yanga

Yondan

KAMATI ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jana ilitoa tamko kuwa, beki Kelvin Yondan ni mchezaji halali wa Yanga.

Tamko hilo limetolewa baada ya kamati hiyo iliyokutana Julai 17, mwaka huu kupitia na kujadili ili kujiridhisha juu ya mikataba ya mchezaji huyo na Simba, ambayo ni timu yake ya zamani.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Alex Mgongolwa, alisema kuwa, kwa mujibu wa mkataba wa Simba na mchezaji huyo ulimalizika Mei 13, mwaka huu, hivyo walichukua uamuzi wa kumruhusu kuchezea klabu ya Yanga, kwani alikuwa mchezaji huru.

Mgongolwa alisema kuwa, Kamati ilibaini kuwa, mkataba uliowasilishwa na Simba TFF, ili kuongeza mkataba wake ulifika Juni 7, mwaka huu, ambapo ni kinyume na taratibu.

Aliongeza kuwa, kutokana na suala hilo, pia mkataba una tatizo la kisheria kufuatia tarehe aliyosaini Yondani ya Desemba 23, mwaka jana, huku Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu,’ aliingia makubaliano hayo Desemba 23, mwaka huu.

Alisema kuwa, kutokana na sababu hizo, Kamati imekubali hatua iliyochukuliwa na Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, kuwa mchezaji Kelvin Yondan kuichezea Yanga katika mashindano ya Kombe la Kagame 2012.

Mchezaji huyo aliibua gumzo baada ya Simba kudai kuwa, Yondan bado ana mkataba na klabu hiyo,  hivyo TFF imeiruhusu Yanga kumsajili kinyume na taratibu za usajili.

Mapema wiki hii, Simba ilidai kukata rufani kwenye kamati hiyo, na kudai kuwa, hili suala linaweza kukatiwa rufani mpaka Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), kupinga usajili wa mchezaji huyo kuichezea Yanga.

No comments