Yanga, Simba vitani kumwania Ngassa
USAJILI wa kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Mrisho Ngassa, umeendelea
kuwa wa simtofahamu, baada ya kuzuka kwa vita ya kumwania nyota huyo kati ya
klabu za Simba na Yanga, ambazo zote zineonesha nia ya kumsajili kwa ajili ya
Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na SuperStar umeonesha kwamba,
timu zote hizo mbili zinazopatikana katika Jiji la Dar es Salaam, zimekuwa
kwenye harakati kubwa za kumsajili nyota huyo ambaye aliwahi kuwika na klabu za
Toto Africans na Kagera Sugar katika miaka ya nyuma.
Imebainika kwamba, Yanga ndio walikuwa wa kwanza kufanya
mazungumzo ya mdomo na baadaye maandishi kwa njia ya barua pepe (email), ili
kufanikisha usajili wa nyota huyo.
Kati ya watu waliohusika na mazungumzo hayo ni Katibu Mkuu
wa Yanga, Mwesigwa Selestine, ambaye alituma barua pepe juzi kwenda kwa Meneja
wa Azam FC, Patrick Kahemele, lakini siku
hiyo hiyo Simba nao walitua Azam FC kwa nia ya kumsajili nyota huyo.
Katika kile kilichoonekana kuwa ni vita kwa pande zote
mbili, Mwenyekiti wa kamati ya usajili wa Klabu ya Yanga, Seif Ahmed ‘Magari’
alifanya mazungumzo na Mmiliki wa Azam, Yusuf Bakhressa na kuanisha kile
walichonacho.
Katika kujua ukweli, SuperStar ilimtafuta, Katibu Mkuu wa
Azam Idrissa Nassor ambaye alikiri kuwepo kwa mazungumzo ya mwisho kati ya Azam
na Simba, ambayo ilionesha nia ya kumsajili Ngassa.
“Suala hili hatutaki kulifanyia mzaha wala kuwa na kificho,
Simba wamekuja na wametoa ofa yao, lakini Yanga hadi sasa hawajafika, hivyo tunazungumza
na mtu aliye mezani na dakika chache zijazo tutakuwa tumeafikiana na Simba.
“Mtoto ameonesha mapenzi ya kwenda Yanga, na sisi tumetoa
ofa, lakini cha ajabu hadi sasa Yanga wamekaa kimya, kwa hiyo hatuwezi
kuwalazimisha,” alisema Nassor ikiwa ni muda mfupi kabla ya kwenda kufuru.
Kutokana na utata huo, SuperStar ilipiga hodi katika kamati
ya usajili ya Yanga, ambapo ilikutana na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Seif Magari
ambaye alikiri kufanya mazungumzo na Bakhressa juu ya usajili wa Ngassa na kukubaliana baadhi ya
mambo muhimu yanayoweza kukamilisha jambo hilo.
“Kweli jana (juzi) usiku nilizungumza na Bakhressa,
nikamweleza kile tulichonacho. Moja ya ofa tulizotoa ni kupewa kwa mkopo au
wakubaliane na dau tulilotoa maana kijana ameonesha nia na mapenzi kwa Yanga.
“Katika mazingira haya, ni wazi kuwa kama kuna mipango ya
kumpeleka Simba, waseme ila tunajua kuwa, hilo haliwezekani, kwani ikumbukwe
kuwa, Azam FC nao wameamua kuuza, baada ya kuonesha mapenzi ya kucheza Yanga,
je? iweje apelekwe Simba, kama alishindwa
Azam tusiokuwa na upinzani nao, ataweza kucheza Simba?
“Kwa busara namshauri Idrissa asikurupuke kuzungumza na
vyombo vya habari, ila afanye mawasiliano na bosi wake (Bakhressa), kwa sababu
tatizo ninaloliona Azam kila mtu ni kiongozi,” alihoji Magari.
Kwa hali hiyo, uchunguzi wetu unaonesha kwamba, ndani ya
Azam kuna tatizo la mawasiliano ambalo limesababisha kuwepo kwa mgongano baina
ya viongozi wake wa juu.
Katika mechi ya nusu fainali kati ya Azam na AS Vita Club ya
DR Congo, Ngassa alifunga bao la ushindi na kuibusu jezi ya Yanga, ambapo
mashabiki walimpa jezi hiyo na kuivaa, hali iliyozusha maswali mengi.
Nyota huyo aliwahi kuzitumikia klabu za Toto Africans ya
jijini Mwanza na baadaye aliunga na Kagera Sugar kisha kutua Yanga ambapo Azam ilimsajili kwa
kitita cha zaidi ya sh milioni 50.
ciao
No comments