Sounders FC kushirikiana na Tanzania
Na Mwandishi Wetu, Washington
TIMU ya Seattle Sounders FC ya
Marekani imetangaza ushirikiano na Tanzania, nchi ambayo ni nchi kubwa kabisa
katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ushirikiano huo ulitiwa saini na
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki (Mbunge) na Mmiliki wa
timu ya Seattle Sounders, Joe Roth, katika hafla fupi iliyofanyika jana mjini
Renton.
Mbali ya Waziri Kagasheki, wengine
walioshuhudia kutiwa saini kwa ushirikiano huo ni Balozi wa Tanzania nchini
Marekani, Mwanaidi Maajar, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania Dr. Aloyce
Nzuki na maofisa wengine kutoka Wizara ya Utalii, ubalozi na
maofisa wa Seattle Sounders FC.
Mambo muhimu katika ushirikiano huo
ni uwekwaji wa alama za vivutio vya utalii vya Tanzania katika maeneo mbalimbali
kama CenturyLink Field na Starfire Sports Complex, uwanja wa mazoezi wa
Sounders FC uliopo eneo la Tukwila.
Vivutio vya Utalii wa Tanzania vitakavyowekwa katika maeneo
hayo ni picha za Mlima Kilimanjaro, hifadhi
za Serengeti, Ngorongoro Crater na Zanzibar.
"Ushirikiano wetu na Bodi ya
Utalii Tanzania (TTB), utasaidia
kutangaza vivutio vya Utalii vya Tanzania nje
ya mipaka yake, kwani kuna vivutio vya ajabu
na kuleta unafuu kwa watalii ,” alisema mmiliki wa timu ya Sounders FC, na
kuongeza kuwa, ushirikiano huo utatoa nafasi muhimu kwa soko la utalii wa
nchini.
Waziri Kagasheki mbali ya kupongeza
kwa kufanikisha hatua hiyo muhimu katika sekta ya Utalii nchini, alisema ushirikiano
huo utatoa fursa nyingi kwa watanzania na wamerekani kwani utaimarisha juhudi
za Wizara ya Utalii katika kukuza soko la utalii wa kimataifa na wa ndani.
Kagasheki pia alisema ushirikiano
huo utatoa fursa za kibiashara kwa nchi zote mbili na kuongeza uwekezaji.
Katika kuhakikisha zoezi la ujumbe
wa kupromoti vivutio vya utalii wa Tanzania vinawafikia wengi, michoro mbalimbali
ya ukutani itachorwa ndani ya uwanja upande wa kaskazini magharibi na kaskazini
mashariki na itaonekana kwa mara ya kwanza kwenye televisheni nchini Marekani, wakati wa mechi ya Sounders FC dhidi ya Chelsea kwenye Uwanja wa
Field CenturyLink Julai 18, wakati Tanzania itakuwa Julai 19.
Pia, maofisa wa TTB watakuwa mbele
wakati wa mkutano wa kabla ya mechi na mashabiki wa soka na kuzungumzia
masuala mbalimbali ya utalii na usafiri katika nchi yao.
Seattle Sounders FC ilianza
majadiliano ya ushirikiano na Tanzania mwaka 2010, ambapo Kocha msaidizi wa
timu hiyo, Kurt Schmid, alikuja nchini katika mpango wa kutafuta vipaji vya
wachezaji.
Mchezaji wa timu ya Taifa, Mrisho Ngassa, wa Azam FC, alisafiri mpaka
Marekani na kucheza mechi ya kihistoria kati ya Seattle Sounders na Machester
United mwaka jana.
No comments