Mchezaji wa zamani wa Simba afariki dunia
KIUNGO wa zamani wa klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam,
Issa Kihange amefariki dunia juzi jioni kwenye mazoezi yaliyofanyika katika
Uwanja wa chuo cha Imtu uliopo Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.
Taarifa zilizopatikana jana zinaeleza kuwa, marehemu Kihange
alikutwa na mauti baada ya kuanguka ghafla uwanjani, wakati akishangilia bao,
ambapo juhudi za kuokoa maisha yake zilifanyika baada ya kufikishwa kwenye Hospitali ya Imtu kwa
matibabu, lakini zilishindikana.
Mwili wa mchezaji huyo ambaye aliwahi kuzitumikia klabu za
Kondoa Rangers, Halmashauri na NBC zote za Kondoa, kabla ya kutua Simba,
umehifadhiwa kwenye Hopitali ya Jeshi Lugalo, huku shughuli za mazishi
zikifanywa na familia yake, ingawa mtu aliyekuwa anasubiriwa kwa ajili ya
shughuli nyingine kuendelea, alikuwa ni mkewe aliyekuwa kikazi jijini Mwanza.
Msiba huo upo nyumbani kwake Mbezi Beach kituo cha Jogoo,
huku taarifa zikieleza kwamb,a anaweza kufasirishwa kwenda Kondoa mkoani Dodoma
kwa mazishi.
Issa Kihange aliichezea Simba kwa mafanikio kati ya mwaka
1989 na katikati ya miaka ya 90 na kufanikiwa kutwaa Kombe la Afrika Mashariki
na Kati ambalo kwa sasa ni Kombe la Kagame mwaka 1991.
No comments