Kilimanjaro Lager yaipa Simba sh. mil. 20 kwa ajili ya mkutano mkuu
Na Mwandishi Wetu
MENEJA wa bia ya Kilimanjaro inayozalishwa na
Kiwanda cha Bia Tanzania (TBL), George Kavishe, jana alikabidhi hundi ya sh.
milioni 20, kwa ajili ya mkutano mkuu wa klabu ya Simba utakaofanyika Agosti 5,
mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kukabidhi hundi hiyo, Kavishe,
alisema kuwa, Kilimanjaro Premium Lager inatambua wajibu wake na
ina nia ya kweli ya kuendeleza soka nchini.
Alisema kuwa, Kilimanjaro inapenda kuona maendeleo
ya klabu ya Simba, ndio maana wameamua kuiunga mkono klabu hiyo ili kufanikisha
mkutano mkuu.
Kavishe alisema kuwa, wanaamini mkutano huo
utaimarisha ushirikiano kati ya viongozi na wanachama kwa kuwapa nafasi ya
kujadili maendeleo ya klabu yao.
“Mtu anapoangalia historia ya klabu hii kongwe
ambayo imejengeka kutokana na rekodi nzuri ya mafanikio kwa muda mrefu, utaona
ina mamilioni ya wapenzi nchini. Soka ndio mchezo unaopendwa sana, na bia ya
Kilimanjaro imekuwa ikitoa mchango mkubwa kusaidia mchezo huu, ambapo leo
tunasaidia mkutano mkuu wa Simba ili kusaidia kudumisha uwajibikaji wa klabu
kwa wanachama wake,” alisema.
Meneja huyo alisema kuwa, wanatambua wajibu wao kama
wadhamini wakuu wa Simba katika kutekeleza mkataba wao, wataendelea kushirikiana
kwa kufanya kazi pamoja ili kuhakikisha soka nchini linazidi kukua.
No comments