Duh! Yanga, yaibamiza APR 2-0
MABINGWA watetezi wa Kombe la Kagame, Yanga, jana ilifanikiwa kuzima kelele za APR ya Rwanda, baada ya kuichapa mabao 2-0, katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Yanga walianza mchezo huo kwa kasi na kulisakama lango la APR, dakika ya tano, Athuman Idd ‘Chuji’, alimjaribu kipa Ndoli Jean kwa shuti kali la mpira wa adhabu lililopanguliwa na kona ambayo haikuzaa matunda.
Shambulizi hilo liliizindua APR, ambapo wachezaji Mbuyi Twite, Seleman Ndikumana na Kabange Twite walijibu mashambulizi, lakini walikumbana na ngome ya Yanga iliyokuwa chini ya Kelvin Yondan na Nadir Horoub ‘Cannavaro’.
Juhudi za Yanga zilizaa matunda dakika ya 22, baada ya Said Bahanuzi kuipatia timu yake bao la kwanza, akitumia vizuri pasi iliyotoka kwa Hamis Kiiza na kupiga shuti kali lililomshinda kudaki kipa Jean na kujaa wavuni.
Bao hilo liliwachanganya APR ambao walifanya mashambulizi ya haraka, dakika ya 32, Olivier Karekezi alishindwa kutumia vizuri mpira uliopigwa na Leonel St. Preus na kuokolewa.
APR wakizidi kulisakama lango la Yanga, walipata nafasi nyingine nzuri kupitia kwa Kabange Twite, lakini shuti lake kali lilidakwa na kipa wa Yanga, Yaw Berko.
Bahanuzi, dakika ya 43, aliwatoka mabeki wa APR na kufanikiwa kuzitikisa nyavu, lakini tayari filimbi ya mwamuzi wa msaidizi kibendera chake kilikuwa juu kuashiria aliotea.
Yanga ambayo jana ilibadilika na kuonesha soka zuri, ilifanikiwa kuwabana wapinzani wao mpaka dakika ya 45 za kwanza zinamalizika ikiwa inaongoza kwa bao moja.
Beki aliysajiliwa msimu huu akitokea Simba, Kelvin Yondan alifanya kazi ya ziada na kuonesha umuhimu wake, baada ya kuondoa hatari langoni, wakati Kabange akiwa amewatoka mabeki wa Yanga na kutaka kumchambua kipa Berko.
Bahanuzi usajili mpya wa Yanga, alikuwa shujaa katika mchezo huo baada ya kuwainua mashabiki wa Yanga vitini kwa kufunga bao la pili dakika ya 66, kwa shuti lililojaa wavuni.
APR ambao walikuwa wakisaka mabao ya kusawazisha, dakika ya 76, walishindwa kuitumia vizuri nafasi waliyopata, baada ya Preus kushindwa kuunganisha mpira akiwa karibu na lango la Yanga na kupiga shuti lililotoka nje ya lango.
Yanga: Yaw Berko, Juma Abdul, Oscar Joshua, Stephano Mwasyika, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondan, Athuman Idd ‘Chuji’, Haruna Niyonzima, Said Bahanuzi/Jerryson Tegete, Hamis Kiiza, Nizar Khalfan/Juma Seif ‘Kijiko’.
APR: Ndoli Jean, Olivier Karekezi, Mbuyi Twite, Seleman Ndikumana, Jean Mugiraneza, Leonel Preus, Johnson Bagoole, Claude Iranzi, Kabange Twite, Albert Ngabo, Donatien Tuyizere.
Katika mechi iliyoanza mapema, URA ya Uganda iliichapa Ports Djibout mabao 3-1, ambayo yalifungwa na Augustine Nsumba, Samwel Mubiru na Feni Ali dakika, wakati bao la Ports lilifungwa na Roland Ayuk
No comments