Header Ads

ad

Breaking News

Kesi ya Hassanoo na wenzake yasogezwa mbele

                                                Hassan Othman 'Hassanoo'

KESI inayomkabili Mwenyekiti wa Chama  cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA), Hassan Othman 'Hassanoo' na Wenzake watatu ya tuhuma za wizi wa tani 26 za madini aina ya shaba yenye thamani ya sh. milioni 400 imeahirishwa hadi Oktoba 12, mwaka huu.

Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya  Hakimu Mfawidhi, Victoria Nongwa, na kusomewa mashtaka  na Wakili wa Serikali, Ladslaus Komanya.

Wakili wa serikali Ladslaus Komanya, aliomba kesi hiyo iahirishwe hadi hapo upelelezi utakapokamilika.

Watuhumiwa wenzake katika kesi hiyo ni Wambura Mahenga (32)MKazi wa Temeke, Dkt. Najimu Msenga (50), mfanyabiashara wa madini mkazi wa kunduchi Mtongani na Salim Shekibula (29), ambaye ni mlinzi na mkazi wa Kunduchi Bahari Beach.

Katika kosa la kwanza ilidaiwa kuwa, washtakiwa Agosti 26, mwaka huu walikula njama  ya kutenda kosa la kuiba vitu vilivyokuwa vikisafirishwa.

Kosa la pili ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, washtakiwa hao waliiba shaba hiyo mali ya Kampuni ya Libert Express(T)Limited iliyokuwa ikisafirishwa na lori T.821ABC lililokuwa na tela T566BCZ likitokea Zambia.

Katika kosa la tatu ilidaiwa kuwa, watuhumiwa hao walipokea  shaba hizo huku wakijua kuwa,  mali hizo zimepatikana kwa njia isiyo halali.

watuhumiwa hao walikana makosa yote waliyosomewa, ambapo wakili wa serikali Komanya alidai kuwa, upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuongeza kuwa, dhamana kwa washtakiwa hao inaendelea.

Kesi hiyo itatajwa tena Oktoba 12, mwaka huu.

No comments